Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Abdi Mahmoud Abdi, amewaelekeza wakandarasi kutoka kampuni Acting Consultancy Ltd wanaojenga Hospitali ya Mkoa ya Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja, kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo kwa kuzingatia makubaliano na muda uliowekwa katika mkataba.
Abdi ametoa agizo hilo akiwa Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja, alipokuwa akiendelea na ziara yake ya kutembelea matawi ya CCM, kukagua uhai wa chama na kusikiliza changamoto za wanachama wa Chama Cha Mapinduzi.
Katika ziara hiyo, Abdi alitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa ya Mahonda, ambapo aliwataka wakandarasi kuhakikisha kazi hiyo inatekelezwa kwa kasi inayokidhi matakwa ya mkataba ili hospitali hiyo ikamilike ndani ya muda uliopangwa.
“Tunawataka wakandarasi wazingatie mikataba waliyopewa. Hospitali hii na miradi mingine ya Serikali lazima ikamilike ndani ya muda uliowekwa kwa mujibu wa mkataba,” alisema Abdi.
Aidha, Abdi aliwaagiza wasimamizi wa mradi huo kufanya ufuatiliaji wa karibu na wa mara kwa mara wa maendeleo ya ujenzi, ili kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinabainika na kutatuliwa mapema bila kusubiri viongozi wakuu kufika eneo la mradi.
“Wale ambao wamepewa jukumu la kusimamia miradi hii wapite mara kwa mara ili kama kuna changamoto ndogo ndogo waweze kuzitatua mapema, badala ya kusubiri viongozi wakuu kufika na kukutana na changamoto ambazo zingetatulika mapema,” alisema.
Alisema, usimamizi madhubuti wa miradi ni muhimu katika kuhakikisha fedha na rasilimali zinazotumika katika miradi ya maendeleo zinatoa matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Abdi pia alisema, CCM itaendelea kufuatilia na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, akieleza kuwa ufuatiliaji huo ni sehemu ya kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM unafanyika kwa kuzingatia mahitaji na changamoto za wananchi.
Alisema, kukamilika kwa Hospitali ya Mkoa ya Mahonda kutasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja katika kupata huduma za afya, hususan huduma za rufaa.
Alisema, kwa muda mrefu wagonjwa wanaohitaji huduma za rufaa kutoka hospitali za wilaya wamekuwa wakipelekwa Hospitali ya Mnazi Mmoja, hivyo uwepo wa hospitali ya mkoa utasaidia kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
Abdi alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa hatua zinazochukuliwa katika kuboresha huduma za afya, ikiwemo ujenzi wa hospitali za mikoa na kuimarisha hospitali za wilaya.
Alisema, hatua hizo zinaendana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na zina lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo wanayoishi.
“Tunampongeza sana Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hususan katika eneo la afya. Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa ya Mahonda ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo yao,” alisema.
Aidha, Abdi alisema kuboresha huduma za afya ni miongoni mwa malengo ya msingi ya Mapinduzi ya Zanzibar, yanayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii.
“Moja ya shabaha za Mapinduzi ilikuwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, ikiwemo huduma za afya. Kwa hiyo kujengwa kwa hospitali hii ya mkoa yenye kiwango na ubora kama huu ni hatua kubwa katika kutekeleza dhamira hiyo,” alisema.
Kwa upande wake Mhandisi Mohamed A. Noor wa Acting Consultancy Ltd amesema ujenzi wa hospitali ya mkoa Mahonda utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 30 hadi kukamilika kwake.