📌 Wanachama, wadau wataka mamlaka ya vikao vya CHADEMA yaheshimiwe
📌Wasisitiza nafasi ya wanaharakati katika siasa, waonya kuhusu mipaka ya ushawishi
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HOJA ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema, kuhusu nafasi ya wanaharakati katika uendeshaji wa vyama vya siasa imepata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya wanachama, wanasiasa na wachangiaji wa mijadala ya kisiasa.
Wakizungumza kwa nyakati na majukwaa tofauti, wadau hao wameeleza umuhimu wa kutenganisha shughuli za uanaharakati na mamlaka ya vyombo rasmi vya chama, wakisisitiza kuwa uamuzi wa kitaasisi unapaswa kufanywa kwa kuzingatia Katiba, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Mjadala umechochewa na kauli ya Lema alipozungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, na kusema CHADEMA ni taasisi ya kisiasa, si chombo cha harakati, huku akitambua mchango wa wanaharakati katika kupigania mabadiliko ya kijamii na kisiasa.
Kwa mtazamo wa Lema, ushirikiano kati ya chama na wanaharakati unaweza kuendelea bila kuathiri mamlaka ya vikao na viongozi wenye wajibu wa kufanya maamuzi kwa mujibu wa Katiba ya chama.
Kauli yake imeibua mitazamo mbalimbali kuhusu nafasi ya wanaharakati katika siasa za upinzani, uhuru wa viongozi kufanya maamuzi na umuhimu wa kulinda misingi ya uendeshaji wa vyama.
Hapi aingia kwenye mjadala
Miongoni mwa waliochangia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ally Hapi, ambaye ameonya kuhusu athari zinazoweza kujitokeza iwapo watu wasiokuwa sehemu ya vyombo rasmi vya chama watakuwa na ushawishi mkubwa katika kufanya uamuzi.
Kupitia mtandao wa X, Hapi ameandika: “Ikiwa CHADEMA haitatoka hadharani na kukataa kuendeshwa kwa rimoti na wanaharakati uchwara, utakuwa ndio mwisho wake. Kansa iliyoanza itawamaliza. Lazima wakate kidole. Chama ni taasisi, Chama ni vikao, Chama ni utaratibu.”
Hapi ametumia dhana ya ‘Party Capture’ kuelezea mazingira ambayo, kwa maoni yake, watu wasiokuwa viongozi au wajumbe wa vikao vinavyotambuliwa na Katiba wanaweza kupata ushawishi mkubwa katika kuamua mwelekeo wa chama.
Amesema vyama vya siasa vinahitaji kulinda mifumo yake ya uongozi ili kuepusha migongano ya mamlaka na changamoto za kiutendaji.
Mdau mwingine, Dkt. Zacky, kupitia mtandao wa X, amesema baadhi ya watu wanaohusika na mijadala ya CHADEMA wanahitaji kutofautisha uendeshaji wa taasisi ya kisiasa na shughuli za uanaharakati.
Alisema viongozi wanaweza kujikuta katika mazingira magumu ya kufanya uamuzi iwapo watahofia kupoteza uungwaji mkono wa makundi yenye ushawishi katika mijadala ya kisiasa.
Ameeleza wasiwasi kuhusu namna viongozi wa chama wanavyokosolewa hadharani, akitaja mijadala iliyomhusu Freeman Mbowe na uwezekano wa viongozi wengine kukabiliwa na mazingira yanayofanana.
Odero apendekeza maridhiano
Mwanachama wa zamani wa CHADEMA, Odero Odero, ameutazama mjadala kwa mtazamo mpana zaidi, akipendekeza chama kuimarisha maridhiano ya ndani na kuweka utaratibu unaolinda uhuru wa uamuzi wake.
Odero amependekeza hatua tatu, ambazo ni kujenga maelewano kati ya makundi mbalimbali ndani ya chama, kuepuka kutegemea ushawishi wa wanaharakati katika maamuzi na kufungua mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na CCM.
Ametaja makundi yanayohusishwa na Freeman Mbowe, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti (John Heche) na Lema, akisema tofauti za kimtazamo zinapaswa kushughulikiwa kwa mazungumzo.
Odero anaamini maelewano yatasaidia kuimarisha mshikamano na kutoa nafasi kwa viongozi na wanachama kujadili masuala yanayohusu mustakabali wa chama.
Pia, amependekeza kuwepo kwa utaratibu wa kuchuja michango ya fedha kutoka kwa wanaharakati, akisisitiza umuhimu wa kulinda uhuru wa chama katika kufanya maamuzi.
Vijana nao wachangia
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) Mkoa wa Kilimanjaro, Achibod Mmbando, amesema vijana wa CHADEMA wana wajibu wa kulinda heshima ya chama na viongozi wake.
Mmbando ameeleza kutoridhishwa na kile anachokiona kuwa mwenendo wa baadhi ya wanaharakati kuhoji uhalali wa viongozi wa chama, akitaka vijana kutambua umuhimu wa kuheshimu mifumo ya uongozi.
“Tofauti za maoni zinapaswa kujadiliwa bila kudhoofisha nafasi ya viongozi waliopewa dhamana kwa taratibu za chama,” alisema.
George Wambura, aliyejitambulisha kuwa mwanachama wa CHADEMA tangu mwaka 2010 na mmoja wa walioanzisha tawi la chama Chuo Kikuu cha St John jijini Dodoma, amesema wanaharakati wana mchango muhimu katika siasa, lakini ushirikiano wao na vyama unahitaji kuzingatia mipaka ya majukumu.
Wambura amesema amekuwa akifuatilia mijadala inayohusu CHADEMA na kubaini changamoto inayoweza kujitokeza pale watu wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii wanapotaka mitazamo yao iwe msingi wa maamuzi ya chama.
Amesisitiza umuhimu wa wanachama kuwa na nafasi ya kujadili na kuamua masuala yao kupitia vyombo vinavyotambuliwa na Katiba.
Uanaharakati na siasa
Mchangiaji mwingine, Esir Idd, amesema mjadala ulioibuliwa na Lema unagusa tofauti ya msingi kati ya mwanaharakati na mwanasiasa.
Kwa maelezo yake, mwanasiasa anawajibika kwa chama, wanachama, sera na wapiga kura, wakati mwanaharakati anaweza kuunga mkono ajenda fulani bila kuwa na wajibu wa moja kwa moja kwa taasisi ya kisiasa.
Idd amesema wanaharakati wana nafasi muhimu katika kuibua matatizo ya jamii, kutetea haki na kuhoji mamlaka, lakini mchango wao haupaswi kuchukua nafasi ya taratibu za kufanya maamuzi ndani ya chama.
Ameeleza kuwa CHADEMA inahitaji kuendelea kujenga sera na dira yake, huku ikitambua umuhimu wa kusikiliza mitazamo tofauti bila kupoteza uhuru wa kimkakati.
Kwa upande wake, Assenga Jr amesema kupigania haki ni sehemu ya uanaharakati, lakini tofauti hujitokeza pale mtu asiye na nafasi katika vyombo vya chama anapotaka kushiriki moja kwa moja katika kufanya maamuzi yake.
Amesisitiza umuhimu wa kutofautisha haki ya kutoa maoni na mamlaka ya kufanya maamuzi ya kitaasisi.
Buyobe atetea mawasiliano
Fortunatus Buyobe ameunga mkono hoja ya Lema kuhusu umuhimu wa mawasiliano katika mazingira tofauti ya kisiasa.
Buyobe amesema wakosoaji wa Serikali wanaoishi nchini na wale walioko uhamishoni wanaweza kutumia mbinu tofauti za kutoa maoni kutokana na mazingira wanayokabiliana nayo.
Ameeleza kuwa watu wanaoishi nchini wanaweza kuchagua lugha na njia za mawasiliano zinazozingatia mazingira yao, wakati walioko nje ya nchi wanaweza kuwa na nafasi tofauti ya kutoa ukosoaji.
Kwa maoni yake, kuwasiliana na watu unaowakosoa hakumaanishi kuacha msimamo, bali kunaweza kuwa sehemu ya mbinu za kisiasa na kulinda mawasiliano.
Buyobe amehitimisha kwa kueleza kuwa anaunga mkono mtazamo wa Lema kuhusu suala la mawasiliano.
Michango ya wanasiasa, wanachama na wadau imepanua mjadala ulioanzishwa na Lema, kutoka nafasi ya wanaharakati hadi masuala ya uwajibikaji wa viongozi, maridhiano ya ndani na uhuru wa vyama kufanya maamuzi.
Pamoja na tofauti za mitazamo, wachangiaji wameweka mkazo katika umuhimu wa kutambua mchango wa wanaharakati katika kudai haki na demokrasia, sambamba na kuheshimu mamlaka ya wanachama na vyombo rasmi vya uongozi wa chama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mwanga na Mjumbe wa Baraza Kuu la CHADEMA Taifa, Lembrus Mchome, amempongeza Godbless Lema, kwa kukemea vitendo vya baadhi ya wanaharakati walioko nje ya nchi, akidai vinachangia kukiharibu chama na kuleta madhara kwa Watanzania.
Mchome alisema, kauli za wanaharakati hao zimeongeza maumivu kwa Watanzania, hasa kufuatia matukio ya Oktoba 29, 2025, yaliyosababisha vifo vya watu, akidai baadhi ya vitendo hivyo vilichochewa na kauli za wanaharakati hao.
Aidha, amemkosoa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa kwa kile alichodai ni kushindwa kujibu tuhuma zilizotolewa na baadhi ya wanaharakati, akisema hali hiyo inaashiria udhaifu wa uongozi na kutokuwepo kwa usimamizi madhubuti wa misingi ya chama.
Alisema, CHADEMA kwa sasa kinaonekana kuendeshwa kwa ushawishi wa watu walioko nje ya nchi, akiwataja akiwemo Maria Sarungi, na kuwataka viongozi wa chama nchini kote kuungana kupinga kile alichokiita kuingiliwa kwa chama na wanaharakati hao.
Katika hatua nyingine, Mchome amemtaja John Heche kuwa miongoni mwa watu anaodai wanachangia kuchelewesha kuachiwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, akisema kuna haja ya viongozi kukaa pamoja kutafuta namna ya kumsaidia mwenyekiti huyo kabla ya hukumu yake.