Na WMA – DODOMA
KIONGOZI mstaafu wa Wakala wa Vipimo (WMA), aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bw. Deogratius Aloyce Maneno amesema uwekezaji wa Serikali katika masuala ya vipimo ndiyo ufunguo wa kujenga uchumi imara na soko la haki.
Alisema hayo Agosti 8, 2026 alipotembelea banda la WMA kwenye Maonesho ya 33 ya Wakulima (Nane Nane), yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Dodoma.
Baada ya kupokelewa na wataalamu wa WMA na kupewa maelezo ya maboresho mapya ya vifaa na elimu ya vipimo, Mkurugenzi Mstaafu alisema anajivunia kuona kazi aliyoshiriki kuianzisha ikiendelea na kukua.
“Nimefurahishwa sana kuona WMA imepiga hatua kubwa. Tulipoanza tulikuwa na changamoto za vifaa na uelewa, lakini leo naona vijana wanasimama wenyewe kutoa elimu. Hii ndiyo tija ya uwekezaji,” alisema.
Kutokana na uzoefu wake wa miaka mingi WMA, kiongozi huyo alitoa ushauri katika maeneo kadhaa ili kuboresha zaidi huduma za uhakiki wa vipimo.
Kwanza, alisema kuwa ni jambo jema kutoa elimu kwa wafanyabiashara wakubwa. Hata hivyo alisisitiza kuwa “huu ni wakati wa kushuka ngazi hadi kwa mama lishe na wauuzaji wa sokoni maana ndio wanaoumia zaidi na vipimo visivyo rasmi,” alisema.
Pia, ‘Bosi Deo’ kama wengi wanavyomwita alitoa ushauri kwa wafanyabiashara kukumbatia teknolojia akisema kuwa “Dunia imebadilika. Tumieni mizani ya kidijitali zaidi na mifumo ya kutoa risiti. Hii itasaidia kuwa na rekodi na kupunguza ubadhilifu katika biashara.”
Aidha, alitoa ushauri kwa watendaji wa WMA kutokuogopa kutumia sheria inayoingoza Wakala kuwabana wale wanaokiuka maelekezo na taratibu halali za kivipimo.
“WMA ina mamlaka. Itumieni. Mkikamata na kutoa faini kwa wale wanaokiuka, wengine watafuata sheria. Soko la haki linahitaji nidhamu.”
Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa WMA, Bi. Veronica Simba, alimshukuru kiongozi huyo mstaafu kwa kuwa sehemu ya walioweka misingi imara ya utendaji kazi WMA.
“Tunajivunia alama ambayo wewe pamoja na wastaafu wengine mliiweka. Leo tunaendeleza dira yenu ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata kipimo sahihi. Milango yetu iko wazi kwa ushauri wako wakati wote,” alisema.
Wananchi waliokuwepo bandani walifurahishwa na uwepo wa kiongozi huyo mstaafu na kusema ni mfano mzuri wa watu kurejea kutoa uzoefu kwa vizazi vipya.
Wastaafu wengine waliotembelea banda la WMA kwenye Maonesho ya NaneNane ni pamoja na Bw. Evarist Masengo aliyekuwa Meneja wa WMA ngazi ya Mkoa na Bw. Joseph Maliti aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi. Wote walikiri kufurahishwa na maendeleo ya Wakala na waliupongeza Uongozi uliopo pamoja na wafanyakazi wote kwa ujumla.