UWT wamchangia Dkt. Mwinyi Milioni 35 za fomu ya urais

0

MKE wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam Mwinyi amewashukuru Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) pamoja na makundi mbalimbali ikiwemo watu wenye mahitaji maalum na wajane kwa kujitokeza kwa wingi kumuunga mkono na kumchangia Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Zanzibar 2025, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Mama Mariam Mwinyi amesema hayo katika hafla maalum ya kumuunga mkono Dkt. Hussein Ali Mwinyi iliyofanyika katika Ukumbi wa Madinat Al Bahr, Agosti 29, 2025.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi amewapongeza Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa kuandaa tukio hilo la kumuunga mkono Dkt. Mwinyi kwa kumchangia Shilingi Milioni 35 kwa ajili ya kuchukua fomu leo katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Vilevile, Mama Mariam Mwinyi amewahimiza wananchi wote kuendelea kudumisha amani na utulivu kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa UWT Zanzibar, Zainab Shomari, alisema wameamua kumchangia Mgombea Urais wa CCM Zanzibar, Dkt. Mwinyi, kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020–2025 na kwamba wanataka aendelee kuimarisha mazuri yaliyopatikana.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda, amefahamisha kuwa wameshawishika na mabadiliko makubwa yaliyofanyika Pemba na Unguja chini ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi na wana kila sababu ya kumchangia na kuendelea kumuunga mkono katika kipindi chote cha Uchaguzi Mkuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here