Utandawazi umekuja na mema na mabaya yake

0

Na Stanislaus Usangira

UTANDAWAZI umeunganisha Mataifa, na umeondoa mipaka kati ya nchi na nchi. Yaani unagusa nyanja zote muhimu, kama vile; uchumi na biashara, teknolojia, siasa na hata utamaduni. Utandawazi umefanya dunia kuwa Kijiji, kwamba matukio mengi yamekua sio ya siri tena.

Kimsingi, maendeleo hayo makubwa yamerahisisha kazi, na hata pia kusaidia katika suala zima la mawasiliano. Sasa si jambo la ajabu kwa mtu wa Tanzania kuwasiliana na mtu wa Kenya, na hata kuwasiliana na mtu wa bara la Ulaya.

Lakini, si ajabu katika ulimwengu huu wa utandawazi ambao umeendelea kiteknolojia, kusikia fulani sasahivi yupo Tanzania na baada ya muda mfupi ukasikia yupo Nairobi – Kenya. Hayo yote ni maendeleo chanya ya utandawazi; yaani usafiri umekua si shida tena, ukingilinganisha na wale wenzetu wa karne za awali.

Sambamba na mchango huo mkubwa wa kimaendeleo katika teknolojia. Lakini, utandawazi kwa upande mwingine umechangia kuleta mmomonyoko wa maadili katika tamaduni zetu hasa kwa vijana. Hakika, ni ugonjwa ambacho umekosa muarobaini wake katika kutibu jambo hilo.

Vijana ndio wanaongoza kwa kufanya mambo ya aibu katika mitandao ya kijamii. Wamekua wakipiga picha za utupu na kuzisambaza mitandaoni; sehemu za siri, zimekua sio siri tena. Ni kinyaa na aibu, lakini hiyo yote ni kwa sababu ya utandawazi na kutaka kuiga mambo ya watu wa Magharibi.

Ukiangalia kwenye Sanaa, hususani muziki (bongo fleva) ndio sehemu ambayo vijana wengi wamekimbilia huko, lakini nako changamoto ni za kutosha. Wasanii wamesahau mavazi ya heshima, nguo zinazotumika katika kurekodia video za nyimbo zao, hakika ni za aibu, lengo la kufanya hayo ni kutafuta umaarufu, na hali wakijua watazamaji wengi ni vijana, na waathirika wakubwa wa utandawazi ni vijana, ndio maana ujinga huo umekua ni mkubwa na unasambaa kwa kasi kubwa.

Ni kwanini basi imekua hivyo? Hiyo yote ni kwasababu wasanii wamesahau lile jukumu lao la kwanza la kuelimisha jamii, na badala yake wamejikita zaidi katika kutafuta maslahi yao binafsi kama vile kujipatia fedha na umaarufu. Kumbe kusambaza viungo vya mwili wao katika mitandao ya kijamii imekua sio shida tena, kwao jambo kubwa ni kujizolea umaarufu.

Katika upande wa elimu, utandawazi umeleta changamoto kubwa hasa kwa vijana wa sasa. Muda mwingi utawakuta na simu au kwenye vijiwe vya kuchezea ‘game’ (play station). Aidha, vijana wengine wanapokuwa darasani wanakosa umakini; utakuta Mwalimu anafundisha, wao wapo ‘bize’ wanachati. Pia, kukua huku kwa teknolojia kumechangia utoro kwa wanafunzi mashuleni, muda mwingine wanautumia kuwa kwenye makundi ya kuangalia mambo yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii, badala ya kuwa mashuleni.

Utandawazi umeua kabisa hofu ya MUNGU na vijana kujiona kuwa wanaweza kila kitu, tazama ongezeko la utoaji wa mimba kwa mabinti linavyokithiri katika kizazi hiki cha digitali. Angalia ukahaba na udada poa ulivyokua sio jambo tena la kuogopwa. Miili imekua sio tena mali ya Mungu badala yake imekua ni sehemu ya kujipatia kipato kwa kufanya ukahaba. Yote hiyo yatokana na kuiga tamaduni za watu wa Magharibi.

Ushoga katika ulimwengu wa sasa umekua kilio kikubwa kwa wahubiri wetu wa makanisa na misikitini. Na wengi wanaojihusisha na shughuli hiyo ni vijana. Ukichunguza kwa umakini, kinachoshawishi kufanya huo ujinga ni kuangalia video za kijinga katika mitandao na kuiga mambo ya huko Magharibi.

Katika suala zima la mavazi ni hatari zaidi. Utandawazi ni kama umekuja kusema kwamba vijana hawaruhusiwi kuvaa nguo za heshima na adabu. Mabinti kuvaa nguo fupi ndo mtindo, na vijana wavulana kuvaa suruali chini ya makalio ndo mtindo wa mjini. Kwa vijana hiyo ni aibu kabisa.

Watu wa Magharibi huvaa nguo nyepesi na fupi kwasababu ya mazingira na hali ya hewa inayopatikana katika maeneo yao. Na zaidi sana mavazi hayo huvaliwa katika msimu husika yaani msimu wa joto. Lakini, kutokana na ufinyu wa uelewa, vijana wetu wamekua wakiiga kila kitu cha mtandaoni hata kama hawafahamu historia au sababu ya kitu hicho kuwepo.

Mitandao ya kijamii badala ya kuwa sehemu ya kusambaza mambo mema, imekua ni sehemu ya kutafutia wachumba kwa vijana. Yaani vijana wakiombana urafiki tu kwenye facebook baada ya wiki moja wamekua wapenzi. Na baada ya wiki tena washapeana mimba na uko ndiko tunazalisha mimba za utotoni, na mwishoni tunakuja kuzalisha watoto wengi wa mitaani. Na mbaya zaidi watoto wanaolelewa na mzazi mmoja na kama sivyo, basi ongezeko kubwa la utoaji wa mimba.

Vilevile, Ukosefu wa ajira, umaskini uliokithiri na uwepo wa utandawizi kumechangia baadhi ya vijana kukimbilia katika wizi wa mitandaoni. Yaani, vijana kutwa wapo bize na simu kujaribu kujipatia ridhiki zao kwa njia zisizo halali. Huko ndiko wale wazee wetu wengi wanaosomesha na hata wale ambao wamekua katika matatizo wamejikuta wakiibiwa na vijana wa aina hiyo.

Kipi kifanyike? Je, Vijana wasijihusishe na mambo ya utandawazi? Jibu, ni hapana. Inafaa kabisa kujiusisha na maendeleo haya ya utandawazi na katika ulimwengu huu wa Sayansi na Teknolojia, kuachana na mambo ya utandawazi hakika ni kuchagua kubaki gizani.

Kikubwa vijana wanapaswa kutambua wanachotaka kufanya na wanachotaka kuiga kutokana na utandawazi. Kupima kwa kina yale yapatikanayo katika mitandao. Maana, ndani ya utandawazi kunaweza kumsaidia mwanafunzi kutumia ‘internet,’ kwa ajili ya kujisomea na kujifunza zaidi kama kijana.

Lakini, kwa kutumia mitandao ya kijamii kama vijana wanaweza kujiajiri uko kwa kutoa mafunzo ya yale mambo mazuri wanayoyajua ambayo wanahisi yanaweza kuleta mchango chanya katika jamii. Ndani ya mitandao ya kijamii humo vijana wanaweza kujuana na watu wengi zaidi na kuongeza idadi ya marafiki na pia kujadilia masuala ya msingi zaidi. Kama vile mbinu za kujikwamua kiuchumi, jinsi ya kupambana na magonjwa kadha wa kadha.

Ni wazi kwamba, kama vijana watachagua sehemu chanya ya utandawazi. kutaleta maendeleo makubwa sana kwa mtu mmoja mmoja na hatimaye kwa Taifa kwa ujumla. Maana kwa nchi zinazoendelea tunahitaji sana teknolojia, mawasiliano na tunawahitaji vijana katika kuendesha teknolojia hizo.

*Mwandishi wa Makala hii anapatikana kwa namba;- 0625 585 018/0694 091 955.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here