Utalii wa kihistoria na mafunzo ya
kumpambanua binadamu

0
DCIM100MEDIADJI_0092.JPG

Na Azadi Mpango

MAISHA ya mwanadamu yamejengwa na historia. Tangu hapo, yeye mwenyewe ni historia. Sio tu kabla ya kuwepo kwake, bali hata kuja na kutoweka kwake katika sayari hii ni historia ambayo huainishwa kama maelezo ya matukio ya wakati uliopita.

Kwa mujibu wa Martin Luther King, binadamu si mtengenezaji wa historia bali ametengenezwa na historia. David Mc Callough (1933), kwa upande wake, aliielezea historia kama ni kitu kinachotuonesha tulipo, na kwa nini tupo.

Kumbukizi na mabaki ya zama za kati na za kale vinabaki kama ushahidi wa uwiano, utangamano na nasaba ya mwanadamu ndani ya historia yake ndefu. Vyote hivyo ni vielelezo vya ukweli kuwa maisha ya mwanadamu ni historia.

Hata hivyo, haitoshi kwa mwanadamu kuyaangalia maisha kwa ainisho la historia pekee bila kujumuisha tafakuri juu ya upande gani sahihi wa historia unaofanya maisha yake yawe na maana na lengo halisi.

Majibu sahihi ya kwa nini mwanadamu alikuwepo na yupo ulimwenguni hayawezi kupatikana bila tafakuri hiyo. Umakini wake katika kuchagua njia sahihi waliyopita wahenga waliosimama katika upande huo sahihi wa historia ndio unaoweza kumsaidia kujua yeye ni nani na yupo ulimwenguni kwa ajili gani.

Sura nzima ya maisha yake itasanifiwa na uchaguzi huo wa njia sahihi. Hapo ndipo anapoweza kujua iwapo yeye ni udongo unaobumbwa na kutoweka bure tu baada ya kipindi fulani cha maisha au ni sanaa endelevu yenye Mbumbaji wa kumwamrisha na kumwajibisha kwa uamuzi wake wa kuchagua njia moja au nyingine ya maisha.

Aidha, atajua papo hapo kama yeye ni udongo wa kutoweka tu ardhini baada ya kumaliza umri wa kuishi au ni mgeni wa nyuma ya pazia la kifo lililofunika siri ya upande mwingine wa maisha yake.

Hapa ndipo kilipo kitendawili kilichoitega akili yake. Ndipo hapa panapoichagiza akili yake kuutafuta undani wa uhai unaokuja baada ya finyango la udongo. Swali linalozaliwa katika mzamo wa tafakuri yake ni kwamba mbona uhai huo hauji kwa ‘mwanakatope’ baada ya mtoto kubumba mwanasesere wake mwenye kichwa, pua, macho, mikono, miguu na viungo vingine?

Mbona uhai huo hauji hata kwenye mdoli uliotengenezwa kwenye viwanda vyenye teknolojia ya hali ya juu Uzunguni? Mbona Masanamu yote ya sanaa ya ufinyanzi ya mwanadamu yamekosa uhai uliomo kwenye finyango la udongo uleule wa kinamo aliobumbiwa mwanadamu? Nani aliyeweka uhai ndani ya finyango la udongo la binadamu?

Kilele hiki cha tafakuri ndicho kitakachoufikia ukweli wa nyuma ya pazia la kifo kwamba, uhai uliokuja kwenye finyango la udongo linalomtaswirisha binadamu haukutoka kwenye tabaka lolote la ardhi. Haukutoka kwenye udongo mwekundu wala mweusi.

Bila uhai huu, hata binadamu naye angekuwa ‘mwanakatope’ tu asiyejitambua kwa lolote mithili ya maiti! Yakini kwamba, nyuma ya pazia la kifo cha mwili wa udongo unaendelea tena uhai inajiri kirahisi moyoni kwa kutambua kuwa uhai huo haukuja kwa mwanakatope kutoka udongoni bali umekuja kwa binadamu kutoka ughaibuni.

Ughaibuni ndio nyuma ya pazia la kifo. Nyuma ya pazia hilo la kuitega akili ya binadamu ndiko iliko nguvu isiyoshindwa kwa lolote. Hiyo ndiyo nguvu inayoleta, inayochukua na inayorudisha uhai. Huo ndio ukweli ndani ya historia.

Kinyume chake, historia huwa uongo mtupu kwa kule kuanza kwake na msingi wa uongo. Historia inayomchora sokwe kama mzazi wa binadamu wa leo lazima izingirwe na uongo kwa sababu ya kuanza kwake na urongo.

Hiyo ndiyo sababu ya wengine kuiogopa historia kwa imani kwamba, imejaa uongo kama alivyopata kusema aliyekuwa kiongozi wa kijeshi wa Ufaransa Napoleon Bonaparte (1769 -1821).

Ushahidi wa kimazingira unasaidia kuchuja ukweli na uongo wa fasihi za warithi waliosimulia na kuandika maisha ya wahenga wa vipindi mbalimbali vya historia.

Kwa kuwa historia imekosa miiko ya kuongopa, kila mmoja huchuna uso na kukaza macho katika kusimulia hata asilolijua. Mwingine huituma mikono yake kutunga ya kutunga na kuisingizia historia.

Kwa falsafa sahihi ya historia, safari na matembezi ya kuitalii sanaa ya maumbile ndani ya jiografia ya nchi moja au nyingine huwa nyenzo muhimu kwa mwanadamu kumtafuta msanii wa Maumbile yanayotuburudisha macho na kutukonga nyoyo mbali ya kutuingizia mapato ya uchumi wa utalii.

Huo ndio mtazamo sahihi juu ya utalii, na kwa mtazamo huo, sote tunalazimika kuwa watalii. Lakini, cha kusikitisha ni kwamba, bado dhana ya utalii imetazamwa kwa macho ya kigeni, na si ya kienyeji. Safari za utalii kwa wananchi zimekuwa za nadra sana licha ya matangazo ya kushajiisha utalii wa ndani.

Kwa jinsi hali ilivyo, wageni hasahasa Wazungu huwa weledi wa historia ya eneo au maeneo ya nchi yetu huku mwanachi tena mwenyeji wa eneo moja au jingine la utalii akikosa hata ulewa mdogo wa eneo lake! Wenyeji walio mbali ndio kabisa huishia kusikia tu.

Miongoni mwa Mikoa yenye mabaki lukuki ya kihistoria nchini ni Iringa uliopata kutawaliwa na Chifu Mkwawa wa Wahehe aliyepambana vikali na wakoloni wa Kijerumani waliojaribu kuutahini uongozi wake wa kimila hasa katika upanuzi wa utawala wao mwishoni mwa karne ya 19.

Kwa mujibu wa historia iliyosimuliwa na kuandikwa, Chifu Mkwawa alizaliwa mwaka 1855, mahali palipoitwa Luhota jirani na Iringa mjini. Jina lake kamili lilikuwa ni Mukwavinyika. Maana ya jina hili la heshima ni kiongozi aliyetwaa nchi nyingi.

Alikuwa miongoni mwa watoto wa Chifu Munyigumba Mwamuyinga aliyerithi uongozi wa baba yake baada ya kushindana na nduguze. Yasadikika kuwa Mkwawa alijiua Julai 19,1898 kuepuka kutiwa mikononi mwa Wajerumani akiwa hai.

Moja ya alama za Utawala wa Wakoloni hao ni Eneo la Kunyongea (Execution Ground) maarufu Kitanzini lililopo Mkoani Iringa ambalo linabaki kuwa mfano wa kumbukumbu za matukio ya kihistoria yaliyotokea mkoani humo katika kipindi cha utawala wa Wakoloni wa Kijerumani katika ardhi ya Tanganyika.

Kuhusiana na eneo hilo ambalo kwa sasa limejengwa mnara wa kumbukumbu, inaelezwa kwamba watawala wa Kijerumani walikuwa wakiwanyonga watu (Wahehe) waliotuhumiwa kutoa taarifa za jeshi au kumuunga mkono Chifu Mkwawa wakati wa vita ya msituni baina ya jeshi la Wajerumani na Mkwawa.

Imeelezwa kwamba, watuhumiwa hao walipigwa risasi na kisha kunyongwa kwa kufungwa kamba ya kitanzi na kuning’inizwa kwenye mti mkubwa uliokuwepo wakati huo katika eneo hilo ambalo kwa sasa linaitwa Kata ya Kitanzini kama kumbukumbu ya matukio hayo.

Lakini, baadhi ya wakazi wa Kitanzini wanasema kwamba, kwa mujibu wa historia wanayoijua wao, wanyongaji walikuwa wawili ambao walifunga kitanzi na kuvuta kamba mmoja huku na mwingine kule ambapo mnyongwaji alikabwa na kitanzi hadi kufa. Mdogo wake Mkwawa, Mpangire Wangimbo, anahesabiwa kama mmoja wa nduguze Mkwawa waliopatwa na mkasa huo.

Ni muhimu kulitembelea eneo hilo kujua matukio ya historia na kujifunza, au pia kutembelea maeneo mengine ya kihistoria Mkoani Iringa, na mikoa mingine. Ni vyema kujua historia ya maisha yetu.

0714 789 265
 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here