MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano nchini, ambapo hadi sasa minara 693 imekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mradi huu sasa umefikia asilimia 91.42 ya utekelezaji wake.
Minara hii imewezesha wananchi waishio maeneo ya vijijini na yenye changamoto za upatikanaji wa mawasiliano kupata huduma muhimu za simu na intaneti.
Hatua hii inachangia kuongeza fursa za kielimu, kiuchumi na kijamii pamoja na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya kidijitali.
Jitihada zinaendelea kuhakikisha minara iliyosalia inakamilika kwa wakati, ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na huduma za mawasiliano bila kujali mahali alipo.
Mradi huu ni sehemu ya malengo ya kimkakati ya Serikali katika kujenga taifa lenye uchumi wa kidijitali na kupunguza pengo la mawasiliano kati ya mijini na vijijini.