Ujenzi daraja la Kinyasungwi – Godegode kuanza Disemba

0

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema, daraja la Kinyasungwi – Godegode lenye urefu wa Mita 154, linalounganisha jimbo la Mpwapwa na Kibakwe mkoani Dodoma litaanza kujengwa ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kukagua barabara ya Mpwapwa-Gulwe – Kibakwe yenye urefu wa KM 48.1 Eng. Kasekenya alisema, Serikali inatambua umuhimu wa daraja Kinyasungwi – Godegode katika barabara hiyo kiuchumi na kijamii, hivyo ujenzi wa daraja hilo utaendana na ujenzi wa barabara unganishi za lami zenye urefu wa Kilomita 6.

“Barabara hii ni muhimu kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na ni kiunganishi kizuri cha mikoa ya Dodoma – Morogoro hadi Dar es Salaam hivyo kukamilika kwake kutaibua fursa za maendeleo kwa wakazi wa Wilaya ya Mpwapwa”, alisema Eng. Kasekenya.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amemtaka mkandarasi Mtwivila Traders anayejenga madaraja madogo katika barabara ya Kongwa – Mpwapwa yenye urefu wa KM 49.19 na mkandarasi Technics Constructions Group anayejenga daraja la Mpwapwa kuhakikisha yanakamilika kabla ya mvua za masika ili kuepusha athari katika madaraja hayo.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Dodoma Eng. Salehe Juma amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa wamejipanga vizuri na ujenzi wa madaraja hayo na barabara unganishi utakamilika kwa wakati na ubora uliokusudiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Josephat Maganga alisema, kukamilika kwa madaraja hayo kutaondoa adha wanayoipata wananchi hususan wakati wa mvua kubwa na kuboresha ustawi wa maisha ya jamii katika eneo hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here