SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inaendelea na kampeni ya elimu kwa umma inayolenga kuwaelimisha wananchi wa maeneo ya vijijini kuhusu miradi ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano, hususan ujenzi wa minara ya mawasiliano, hasa katika maeneo yao.

Kupitia kampeni hiyo, wananchi wanaelezwa uwekezaji unaofanywa na Serikali, faida za huduma za mawasiliano katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, pamoja na umuhimu wa kushiriki kulinda miundombinu ya mawasiliano katika maeneo yao.
Kampeni hiyo inatekelezwa kwa mikutano ya hadhara, mazungumzo ya mtu mmoja mmoja ama vikundi vya kijamii kwa kushirikiana na viongozi wa kata na vijiji ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kushiriki kikamilifu katika miradi ya mawasiliano.
