Mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Selasini.
Na Jumbe Abdallah
MWANASIASA mkongwe ambaye ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Selasini amekishauri chama chake kuingia kwenye mchakato wa maridhiano.
Akizungumza na gazeti hili jana, Selasini alisema anaunga mkono kuanza kwa mchakato wa maridhianoi ili kuwaunganisha watanzania kwa kuondoa tofauti zao.
Alisema, mchakato wa maridhiano unaanza na uteuzi wa wajumbe ambao wanakwenda kusimamia zoezi hilo, hivyo haoni sababu za chama chake kukataa, kwani kama kuna hoja za kupinga basi zitaonekana mbele wakati mchakato huo ukiendelea.
“Mimi ni mwanachama wa kawaida wa Chadema na chama kina msemaji wake, ila msimamo wangu binafsi naona kuzuia chama kuingia kwenye mchakato ni kama kuzuia gari kwenda mbele, lazima tuingie kwenye mchakato wa maridhiano kwanza kisha kule mbele tunaweza kutoa hoja zetu tunazoona kwamba lazima zitekelezwe,”
“Mfano mchakato huo wa maridhiano utakapoanza zinaweza zikaibuka hoja ambazo sisi Chadema tukasema hizi zinaweza kujibiwa na Mwenyekiti wetu Tundu Lisu pekee kwa hiyo mwachieni aje ajibu hizi hoja na anaweza akaachiwa kwa njia hiyo,” alisema.
“Lakini kulazimisha Lisu atoke kwanza ndipo twende kwenye mchakato wa maridhiano mimi naona siyo sahihi hata kidogo sana sana naona kugomea mchakato wa maridhiano ni kuendelea kumtesa Mwenyekiti wetu Lisu,” alisema.
Selasini alisema, maridhiano ni suala muhimu kwani kama kuna mgawanyiko kwenye jamii kuna uwezekano mkubwa mipango mingi ya maendeleo isitekelezeke.
“Mimi naona maridhiano ni ya Watanzania wote isipokuwa vyama ni muhimu zaidi kwasababu vinauwakilishi mpana zaidi ndiyo maana vinatajwa kwenye suala la maridhiano, maridhiano ni tunda la mchakato mimi nasema huwezi kuwa na maendeleo kama kuna mgawanyiko,” alisema.
“Turuhusu mchakato wa maridhiano uanze kwasababu ukisema huingii kwenye maridhiano wakati ni tunda la mwisho, mimi hapo nashangaa, lazima tuingie kwenye mchakato wenyewe, tukikuta ajenda haziko sawa ndipo tunatoka,”
“Mfano mnaingia kwenye mchakato mnakuta wajumbe wengine ni wale waliosababisha mgawanyiko huu kwa hiyo mnakuwa na haki ya kuwakataa lakini ukisema huingii wakati mchakato haujaanza sasa unakataa nini,” alihoji
Kwa upande wake mwanasiasa mkongwe nchini, Wilfred Rwakatare, amesema kwa siasa za kidunia maridhiano hayaepukiki, hivyo Chadema lazima wakubali kukaa mezani na kufikia maridhiano.
Akizungumza jana Julai 15, 2026, jijini Dar es Salaam, Rwakatare ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Bukoba Mjini kwa tiketi ya (CUF) na kwa Awamu nyingine akiwa Chadema, alisema kwa siasa za sasa hakuna namna unavyoweza kuepuka suala la maridhiano.
“Kama Mataifa makubwa kama Marekani na Iran yanapigana na yanafikia wakati yanasema tuache vita tuzungumze maana yake ni kwamba, kila jambo lazima lifike mwisho, kama kupigana mtapigana mpaka lini si bora mkae mezani myamalize,” alisema.
“Ila kukifanyika maridhiano lazima kuweka na utashi wa kisiasa wa kutekeleza yale ambayo mmeamua kuridhiana, mimi binafsi naunga mkono maridhiano, ndiyo siasa za kidunia zinavyotaka kwasababu kila jambo si lazima lifikie kikomo, hakuna hali ya kudumu milele wakae wazungumze,” alisema.
“Labda Chadema wanasita kwasababu wanaona ajenda zao za kwenda kwenye maridhiano haziuziki maana kwenye maridhiano lazima ajenda za pande zote ziwe zinanunulika kisha mnakaa katikati mnazungumza mambo yanaisha tunasonga mbele,” alisema Rwakatare.