Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya.
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameielekeza Taasisi ya Vikosi vya Ujenzi kujiendesha kwa misingi ya kibiashara ili kuongeza ufanisi, ushindani na mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Mhandisi Kasekenya ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ofisi za Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) jijini Dodoma, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi.
Amesema taasisi hiyo ilianzishwa kwa lengo la kufanya shughuli za kibiashara, hivyo Serikali inatarajia kuona mchango wake ukiongezeka katika kukuza uchumi wa taifa kupitia uwekezaji, ujenzi wa miundombinu, utoaji wa ajira na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Taasisi hii ilianzishwa rasmi kwa ajili ya kufanya biashara. Serikali inataka kuona matokeo yake yakijidhihirisha katika kuchangia maendeleo ya taifa kupitia uwekezaji, ajira na utekelezaji wenye tija wa miradi ya maendeleo,” amesema Mhandisi Kasekenya.
Ameongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaweka msisitizo mkubwa katika kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za maendeleo, hivyo ameishauri taasisi hiyo kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kuongeza tija, ushindani na ubunifu.
Aidha, ameielekeza taasisi hiyo kupanua wigo wa shughuli zake kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali, ikiwemo TANROADS, pamoja na kuongeza juhudi za kuitangaza ili wadau wengi zaidi wafahamu uwezo na huduma zake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Vikosi vya Ujenzi, Mhandisi Simeoni Machibya, amesema taasisi hiyo inaendelea kutoa mchango katika kukuza uchumi wa taifa kupitia ulipaji wa kodi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Taasisi ya Vikosi vya Ujenzi inatekeleza jumla ya miradi 25, ambayo inasimamiwa kwa karibu ili kuhakikisha inakamilika kwa ubora, kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Mhandisi Machibya ameongeza kuwa taasisi hiyo inaendelea kushindana kwa ufanisi na makampuni ya Serikali pamoja na yale ya sekta binafsi katika sekta ya ujenzi.