Na Mwandishi Wetu
SERIKALI kupitia mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umetoa vifaa 250 vyenye thamani ya Shilingi Milioni 261 kwa ajili ya kuhakikisha Shirika la Posta nchini linatoa huduma zake Kidigitali.
Hayo yamesemwa jana, Mei 26, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Mhandisi Peter Mwasalyanda katika kikao kazi na Wahariri na Waandishi wa habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilikuwa na lengo la kutoa elimu na kuonesha mafanikio yaliyopatikana kupitia UCSAF katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mwasalyanda alisema, vifaa hivyo vilitolewa kwa ajili ya kusaidia ufikishaji wa mizigo na barua majumbani, ambapo mwezi ujao (Juni, 2025) wanatarajia kutoa vifaa vingine 250 kwa Shirika hilo ili kuwafikia watu wengi zaidi kwenye mikoa yote nchini, ambapo huo ni kati ya miradi ambayo wanaitekeleza kwenye maeneo mbalimbali.
Akitaja miradi mingine, Mhandisi Mwasalyanda alisema, wanaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa minara 758, ambapo Mei 2023, Serikali kupitia UCSAF iliingia mikataba na watoa huduma kufikisha mawasiliano maeneo ya vijijini na kata 713 zitanufaika kupitia minara hiyo.

Mbali na kata hizo, alisema halmashauri za wilaya 127 ndani ya mikoa 26 itanufaika ambapo wananchi Milioni 8.5 watafikiwa na huduma za uhakika za mawasiliano, ambapo kupitia mradi huo, Serikali imetoa ruzuku ya Shilingi Bilioni 126 ili kuufanikisha.
Mradi mwingine wanaotekeleza ni ufungaji wa huduma za intaneti ya bure katika maeneo ya wazi, ambapo hadi sasa wamefunga katika vituo saba nchini na maeneo 17 katika viwanja vya Maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Aidha, mfuko huo unaendelea kuwajengea walimu uwezo ili waweze kuwafundisha kwa ufanisi wanafunzi kuhusu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na tayari walimu 3,798 wamepatiwa mafunzo hayo kutoka shule 1,791 za sekondari nchini.

“Lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo walimu na kutatua matatizo ya vifaa TEHAMA, tayari walimu 3,798 wamepata mafunzo hayo katika shule 1,791. Kwa Zanzibar walimu ni 326 na Tanzania Bara walimu ni 3,180 na mafunzo hutolewa pale DIT, UDOM na MUST,” alisema.
Mhandisi Mwasalyanda aliendelea kusema: “Katika kipindi cha miaka minne ya Awamu ya Sita walimu 1,585 wamepata mafunzo ya TEHAMA. Pia, mfuko umeanzisha utaratibu wa kuwachukua wanafunzi wa kike wakati wa likizo na kuwajengea uwezo kuhusu TEHAMA katika maeneo maalum.”

Alisema, lengo ni kupata wabunifu wengi wa kike na kuongeza wataalamu wa TEHAMA nchini. Wanafunzi kutoka shule zaidi ya 300 nchini wamenufaika. Pia, kuna mradi mwingine wa kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za wenye mahitaji maalum.
“Kwa sasa, shule 22 zimeshanufaika kupitia mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 1.8 nchini,” alisema na kuongeza kuwa, vifaa vilivyopelekwa kwenye shule hizo ni TV, Braille Machine (Nukta Nundu) Orbit reader (Machine za Kisasa), Laptops, Embosser (Printa ya nukta nundu), Digital voice recorders na Magnifiers.