MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa jitihada kubwa za kuimarisha utendaji wa Sekta ya Bandari nchini unaowezesha ufanisi wa huduma za kibandari zenye Mchango mkubwa katika ukusanyaji wa Mapato ya Serikali.
Pongezi hizo zimetolewa na Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda alipotembelea Bandari ya Tanga akiongozana na Mwenyeji wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA Plasduce Mbossa na kushuhudia mageuzi makubwa katika Bandari hiyo kufuatia uwekezaji uliofanywa katika miundombinu na vitendea kazi Bandarini hapo.
Mwenda alisisitiza umuhumu wa ushirikiano kwa Taasisi hizi mbili katika kufanya kazi pamoja, kuongeza ufanisi wa huduma zake na Mchango wake katika Maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu TPA, Plasduce Mbossa amepongeza ushirikiano uliopo baina ya TPA na TRA na kuahidi ushirikiano huo kuimarishwa zaidi hasa katika eneo la matumizi ya TEHAMA ili kupata usahihi wa taarifa za Shehena na tozo zinazostahili kutozwa.
Aidha, Viongozi hao walipata fursa ya kutembelea Bandari za Pangani na Sahare na kujionea utoaji huduma na kujadiliana namna bora ya kuongeza wigo wa ukusanyaji Mapato katika Bandari hizo ndogo.