Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Mpira wa miguu ya Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Kombe la Mashindano ya Wafanyakazi (Dar es Salaam Staff Sports League – DSSL).
TRA SC walitwaa ubingwa huo kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) waliokubali kichapo cha bao moja bila.
Mchezo huo ambao umechezwa katika uwanja wa TRA Kurasini, Aprili 5, 2025 ulishuhudiwa na shamrashamra na shangwe mbalimbali kwa mashabiki wa timu zote mbili.

TRA SC walifanikiwa kupata bao kipindi cha pili, na lilidumu mpaka mwisho wa mchezo huo, na kuwafanya kuwa mabingwa wapya wa kihistoria kwa kutwaa mfululizo, wakifanya hivyo mwaka jana 2024, na mwaka huu 2025.
TRA pia wameweka rekodi ya kipekee kwa upande wa timu ya Wanawake ya mchezo wa Netball ambapo walitwaa ubingwa dhidi ya Timu ya Wanawake ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na kuifanya kuwa mabingwa kwa mara ya pili mfululizo.
Awali, akikabidhi zawadi za ushindi, Mdau wa Michezo na Mwanamichezo nchini Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, Dkt. Jonas Tiboroha kwa niaba ya Mkurugenzi wa Michezo BMT, alipongeza vipaji vya wachezaji wa timu zote huku akiomba maafisa Uajili kuendelea kuwekeza zaidi michezoni kwani inasaidia Wafanyakazi kuwa vyema kiafya na ufanisi kazini.
“Niwapongeze viongozi wa timu zote bahati nzuri mpo hapa. Michezo inasaidia ufanisi, inapunguza hata bajeti ya matibabu, tuendelee kuwekeza kwenye michezo na tuangalie namna ya kuweka sawa Miundombinu ya michezo,” alisema Dkt Tiboroha.

Aidha, aliipongeza TRA kwa ujenzi wa uwanja huo wa Kurasini jambo linalowapa ufanisi mkubwa kwa kushinda makombe katika michuano mbalimbali ikiwemo SHIMUTA na mingine mingi ya Wafanyakazi nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ligi hiyo, Japhari Saidi Mtoro amezipongeza timu zote kwa hatua waliofikia, huku akiahidi msimu ujao mambo makubwa.
“Mashindano ya wafanyakazi lazima yalindwe kwa nguvu na wivu mkubwa, hivyo ni muhimu kuwekeza katika mifumo itakayozuia mtu yeyote asiye na sifa kushiriki mashindano hayo.
Akifafanua zaidi Mwenyekiti amesema kuanzia msimu unaokuja wataweka mfumo wa biometric utakaotumika kuwasajili na kuwatambua wachezaji kwa sura zao na alama za vidole.
Mashindano hayo yalishirikisha timu 14, zilizocheza mfumo wa Ligi, kila wiki ilikujenga Afya ya Watumishi wachezaji maofisini, lakini pia kujiandaa na michezo mbalimbali pahala pa kazi.