MKURUGENZI wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndunguru ametaja mambo sita ambayo yanaweza kukifanya Kilimo kuwa na Tija na kuchangia zaidi uchumi wa nchi.
Prof. Ndunguru wakati akizungumza kwenye mkutano na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, jijini Dar es Salaam alisema miongoni mwa mambo hayo, ni suala la utafiti ambalo ni muhimu kwenye sekta ya kilimo na wao wamekuwa wakilipa kipaumbele.
Alisema, viwanda vingi hapa nchini vinategemea Malighafi kutoka kwenye kilimo, hivyo ni vema sekta hiyo ikaboreshwa ili kuchangia zaidi uchumi wa viwanda ambayo ni moja ya sera za nchi.
Prof. Ndunguru alisema, kwa kulitambua hilo Serikali imetenga bajeti kubwa kwenye Sekta ya Kilimo, ambapo imefikia Shilingi Bilioni 970.78 na nguvu kubwa imeelekezwa kwenye utafiti wa mbegu bora, uzalishaji wa mbegu na miche bora, usambazaji wa mbegu na miche ya ruzuku sambamba na kuboresha miundombinu ya kilimo.
Jambo jingine alisema, inatakiwa kufanyike kilimo kinachotumia Sayansi, Teknolojia za Kisasa zitakazosaidia kukusanya takwimu na ubunifu ambao utasaidia kuinua zaidi sekta hiyo na kuchangia uchumi wa nchi.
Aidha, Prof. Ndunguru alisema katika harakati za kuleta mageuzi ya kilimo nchini, ni muhimu kukaimarishwa mahusiano baina ya Serikali na sekta binafsi, na hapo alisisitiza zaidi diplomasia ya uchumi. “Bila kuwa na mahusiano mazuri na nchi nyingine au kuwa na diplomasia nzuri, hatuwezi kuwa na tija kwenye kilimo.”
Suala jingine alisema, ni vema miundombinu ya kilimo ikaboreshwa ikiwemo kwenye kilimo cha umwagiliaji na usafirishaji wa mazao, vile vile kuwezesha biashara ya kilimo.
“Sita, ili tuwe na Mageuzi kwenye kilimo na kuwa na kilimo chenye tija, ni vema tukapunguza upotevu wa mazao kabla na baada ya kuvuna, vyote hivi vinaenda kuleta faida kubwa katika kilimo an kuchangia uchumi wa nchi,” alisema Prof. Ndunguru.