Na Mwandishi Wetu
KAMISHNA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware amesema, mteja yeyote ambaye hatoridhishwa na mchakato wa malipo ya BIMA yake, anapaswa kufikisha malalamiko yake kwenye taasisi hiyo ili asaidiwe.
Dkt. Saqware ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam mbele ya wahariri na waandishi wa habari.
“Ukipata matatizo katika ulipwaji wa huduma ya BIMA, tunakukaribisha kwenye mamlaka yetu tukusaidie,” alisema.
Alisema, sehemu ya kazi ya taasisi hiyo ni kuhakikisha inalinda haki ya mtoa huduma na mteja wa huduma hiyo.
Pia alisema, tayari TIRA imetoa mwongozo kuhusu muda wa kujibu maombi ya mteja kwa kampuni yake inayomuhudumia.
“Awali hakukuwa na muongozo wa mteja wa BIMA kupata huduma ndani ya muda fulani, lakini tumetoa muongozo huo.
“Mteja akidai leo, kampuni inapewa siku saba kumjibu. Akipeleka nakala zake tunampa siku 14 kueleza namna atavyomuhudumia na kama anaona hana vigezo basi aeleze,” alisema na kwamba mteja asiporidhika anapaswa kwenda TIRA.
Kamishna huyo alisema, tayari kuna mwongozo maalumu wa namna ya kujua kiwango cha mtoa huduma anapaswa kutoa kwa mteja wake.