TFS yaweka mkakati wa kukabiliana na hatari zinazotishia misitu

0

Na Mwandishi Wetu, Iringa

KATIKA ukumbi wa VETA uliopo katikati ya Manispaa ya Iringa, maafisa na askari wa misitu walikusanyika Agosti 25, 2025, wakiwa na dhamira ya kuhakikisha misitu ya Nyanda za Juu Kusini inalindwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) – Kanda ya Nyanda za Juu Kusini umefungua rasmi kikao kazi cha kuhuisha Daftari la Viashiria Hatarishi (Risk Register) kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Ni kikao kinachoangalia si tu changamoto zilizopo, bali pia kinatabiri hatari zinazoweza kuathiri malengo ya uhifadhi na kuzitafutia suluhu mapema.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhifadhi Mkuu Daraja la Kwanza kutoka TFS Makao Makuu Dodoma, Marium Mrutu, alisema lengo kuu la mchakato huu ni kutambua mapema hatari zinazoweza kuathiri kufikiwa kwa malengo ya taasisi, kuzipima na kuweka mikakati ya kudhibiti au kupunguza madhara yake.

“Tunapopima hatari mapema, tunajipa nafasi ya kuzuia hasara kubwa. Hii ndiyo njia bora ya kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha misitu inawanufaisha Watanzania wote,” alisema.

Mafunzo haya pia yamewezeshwa na PCR Roland Peter Mlingi kutoka TFS Kanda ya Mashariki, ambaye alisisitiza umuhimu wa taasisi za umma kuimarisha Risk Register kila mwaka ili kuongeza uwajibikaji na kuimarisha utawala bora.

Kwa mujibu wa Mrutu, hatua hii ni zaidi ya utaratibu wa kiutawala. Ni dhihirisho la dhamira ya kulinda rasilimali za misitu kwa manufaa ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.

Hatua hii inalenga kuongeza uimara wa mifumo ya usimamizi wa misitu, kuhakikisha mapato ya serikali hayapotei, na kuendeleza ushirikiano na jamii zinazozunguka hifadhi.

Kikao hiki ni kielelezo cha namna ambavyo taasisi za umma zinavyoweza kujenga misingi ya uthabiti na utawala bora, zikihakikisha rasilimali adimu za taifa hazipotei mikononi mwa kizazi cha sasa, bali zinabaki salama kwa mustakabali wa vizazi vijavyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here