TFS wajivunia mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia

0
Kamishina Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo.

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), umeweka wazi kwamba, miaka mitatu ya Utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, umekuwa chachu ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya hifadhi ya misitu nchini.

Kamishna Mkuu wa Uhifadhi (TFS), Prof. Dos Silayo Santos, alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Prof. Santos alisema, Rais Dkt. Samia, amefanya kazi kubwa ya kuongoza nchi ikiwemo kuboresha Sekta ya Maliasili na Utalii ambapo kwa kipindi alichokaa madarakani, TFS wamefanikiwa katika maeneo 12.

Alisema, miaka mitatu ya Rais Samia madarakani imesaidia kuongeza Rasilimali Misitu 464 ambayo inasimamiwa na TFS, ambapo inasimamia misitu 464 ya Hifadhi inayojumuisha mashamba ya miti 24, misitu ya mazingira asilia, misitu yote ya mikoko kwenye mwambao wa Pwani ya Bahari.

Akitaja maeneo ambayo wamefanikiwa kwa kipindi hicho ni pamoja na Usimamizi wa rasilimali watu, ambapo TFS inasimamia rasilimali watu wanaojumuisha maofisa 643 na askari 1,454 jumla yao ikiwa ni 2097 katika kipindi cha Mwaka 2020/21.

“2023/2024 TFS iliajiri watumishi wapya 495. Watumishi 180 walipatiwa mafunzo ya muda mrefu na watumishi 1,481 ya muda mfupi katika fani mbalimbali,” alisema Prof. Santos.

Mafanikio mengine ni usimamizi wa rasilimali za misitu, usimamizi na uendelezaji wa mashamba ya miti ya Serikali, kwenye eneo hilo alisema wamefanikiwa kutatua migogoro 423 kati ya 438 baina ya hifadhi na vijiji na vitongoji.

Alisema, wamefanikiwa kutoa eneo la hifadhi yenye hekta 296,881 kwa ajili ya makazi, kilimo na ufugaji kwa wananchi, sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi na usimamizi wa misitu: “tumeimarisha mipaka kwa kuisafisha, kuweka vigingi na mabango ili kuzuia uvamizi katika maeneo ya hifadhi.”

Vile vile, Prof. Santos alisema wamefanikiwa kufanya uhakiki wa mipaka ya misitu 55 yenye ukubwa wa hekta 1,453,025.846 “Pia misitu nane yenye ukubwa wa hekta 483,508.4 ilipandishwa hadhi kuwa hifadhi za misitu ya Mazingira Asilia, misitu hiyo ni Itulu Hills Pindiro, Pugu – Kazimzumbwi, Uzigua, Essimingori, Uvinza, East Matogoro na Hasama Hillls.”

Prof. Santos alisema, tathmini ya rasilimali za misitu ilifanyika katika misitu 133 yenye ukubwa wa hekta 2,539,095.04 na kuandaliwa Mipango ya usimamizi (management plans) ambapo juhudi hizo zinaendelea na katika mwaka wa fedha 2023/2024 itaandaliwa mipango ya misitu 56 yakiwemo mashamba ya miti 14.

Mbali na hayo, TFS wamefanikiwa kukabiliana na majanga ya moto yanayojitokeza kwenye mapori mbalimbali, na wamefanya jithada za kujikinga na moto katika hifadhi za misitu ikiwemo kusafisha mipaka na njia za moto zenye urefu wa Kilomita 13,426 pamoja na kutoa mafunzo ya mbinu za kukabiliana na kuepusha matukio ya moto kwa wananchi zaidi ya 29,685 katika vijiji 749 vinavyozunguka misitu 120.

Mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuendeleza utalii Ikolojia na utamaduni, ufugaji nyuki, ukusanyaji wa maduhuli na mchango kwenye mfuko mkuu, maendeleo ya viwanda na biashara sambamba na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema, Wakala umekusanya Shilingi Bilioni 371.9 na kufanikiwa kutoa gawio kwa Serikali kiasi cha Shilingi Bilioni 62.9 ikiwa ni asilimia 15 ya makusanyo.

“Pia, tumeimarisha mazingira ya kazi ambapo katika kipindi cha miaka mitatu Wakala umenunua vyombo mbalimbali vya usafiri na mitambo yakiwemo magari 113, pikipiki 164, mitambo 17 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 18,” alisema.

Aidha, Wakala umejenga majengo 88, zikiwemo ofisi 33, nyumba za watumishi 29, vituo vya ulinzi 26 na maghala ya kuhifadhia silaha nane na ujenzi wa mifumo na Matumizi ya TEHAMA.

Prof. Santos alisema, kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia, TFS wamefanikiwa kuwashirikisha wadau katika uhifadhi, utalii na elimu kwa umma, huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya Taifa.

Alisema, kutokana na jitihada zilizofanyika, wamefanikiwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vituo vya utalii Ikolojia kutoka 59,606 mwaka 2020/2021 hadi 242,824 mwaka 2022/2023 na mapato katika kipindi hicho yaliongezeka kutoka Shilingi 154,965,050 hadi kufikia wastani wa Shilingi Bilioni 1.5.

“Haya ni mafanikio makubwa kupatikana na Wakala katika sekta ya utalii eneo la utalii ikolojia kuliko wakati mwingine wowote. Wakala umejiwekea malengo ya kuweka rekodi mpya kwa kufikisha watalii 500,000 na kukusanya Shilingi Bilioni Tatu ifikapo mwaka 2025,” alisisitiza Prof. Santos.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here