Na John Mapepele, Geneva, Uswisi
TANZANIA imethibitisha tena dhamira yake ya kuimarisha huduma za Kinga, Uchunguzi, Tiba na Uangalizi wa Saratani kufuatia kutolewa kwa Ripoti ya Uhakiki wa Misheni ya imPACT 2025, huku Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, akiahidi kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Kimataifa wakati wa kikao cha pande mbili kilichofanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 79 wa Shirika la Afya Duniani (WHA) mjini Geneva.
Akizungumza katika kikao hicho, Mchengerwa alisema kuwa, Serikali ya Tanzania inathamini ushirikiano wake wa muda mrefu na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), hasa katika kupanua huduma za Saratani na kuimarisha mfumo wa afya kupitia matumizi salama na ya amani ya Teknolojia ya Nyuklia.
“Hii ni mara ya pili mwaka huu kukutana na Viongozi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki,” alisema Mchengerwa, akibainisha kuwa mazungumzo yaliyofanyika mwezi Februari 2026 yalijikita katika ushirikiano wa kimkakati kwenye huduma za Saratani, ikiwemo uwezekano wa kuanzishwa kwa Kitengo cha Kikanda cha mafunzo na huduma za pamoja.
Waziri huyo alieleza kuwa, Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na IAEA kupitia zaidi ya miradi 12 ya afya inayolenga kuboresha huduma jumuishi za Saratani.
Miradi hiyo inahusisha kuimarisha mifumo ya taarifa za Saratani, kampeni za kinga na uhamasishaji, kujenga uwezo wa Wataalamu pamoja na kuboresha upatikanaji wa vifaa vya uchunguzi na matibabu.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, Tanzania pia imenufaika na Mpango wa Ushirikiano wa Kiufundi wa IAEA, ikiwemo kushiriki katika tathmini ya imPACT pamoja na mpango wa Rays of Hope, ambayo inalenga kuimarisha huduma za kudhibiti Saratani Barani Afrika.
Misheni ya Uhakiki wa imPACT 2025 ilifanya tathmini ya uwezo wa Tanzania katika huduma za Saratani katika mnyororo mzima wa huduma, na kuwa tathmini ya pili kubwa kufanyika nchini ndani ya karibu muongo mmoja.
Ripoti hiyo inatoa tathmini huru inayotegemea ushahidi kuhusu maendeleo yaliyopatikana pamoja na kubainisha maeneo ya kipaumbele yanayohitaji hatua za haraka.