NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameongoza ujumbe wa Mawaziri wa Tanzania na kuwasilisha hotuba ya nchi katika Mkutano wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jijini Arusha.
Mkutano huo umefanyika Julai 10, 2026 katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha na umewakutanisha mawaziri na viongozi wa sekta husika kutoka nchi wanachama kwa lengo la kujadili maendeleo ya miundombinu na ushirikiano wa kikanda.
Akitoa hotuba yake katika mkutano huo, Mhandisi Kasekenya alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa EAC katika kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafishaji,mawasiliano na huduma za hali ya hewa ili kuchochea biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa ukanda huo.
Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya wataalamu na makatibu wakuu vilivyojadili masuala mbalimbali ya miundombinu ya usafiri ikiwemo barabara, reli, bandari, usafiri wa anga, vituo vya huduma za pamoja mipakani (OSBPs), mawasiliano na hali ya hewa.
Pia kikao hicho cha ngazi ya Mawaziri kilipokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa miradi na programu za kikanda, pamoja na utekelezaji wa maamuzi na maelekezo yaliyotolewa na vyombo vya kisera vya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, mkutano huo umejadili maendeleo ya programu ya ushirikiano wa Jumuiya tatu za COMESA, EAC na SADC inayolenga kuimarisha usafiri, biashara na maendeleo ya kiuchumi katika kanda ya Afrika Mashariki na Kusini.
Miongoni mwa viongozi wa Tanzania waliohudhuria mkutano huo ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Zakaria Mkama na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya.
Mkutano huo unatarajiwa kutoa maelekezo yatakayosaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu katika nchi wanachama wa EAC.