Geneva, USWISI
TANZANIA imeandika historia baada ya kutunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya WSIS Prizes 2026 kupitia mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano, uliopanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini yaliyokuwa hayana huduma nchini.
Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki katika hafla iliyofanyika Geneva, Uswisi, Julai 10, 2026.
Utambuzi huo unaonesha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kuharakisha ujumuishaji wa kidijitali nchini.
Mradi wa Minara 758 ulitekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kushirikiana na kampuni za mawasiliano za YAS, Vodacom, Airtel, TTCL na Halotel.
Mradi huo umefikisha huduma za mawasiliano katika vijiji 1,400 na kuwawezesha wananchi zaidi ya milioni 8.5 kupata huduma za mawasiliano.
Hatua hiyo imeongeza fursa za biashara, elimu, afya, huduma za kifedha na huduma nyingine za kijamii kupitia teknolojia za kidijitali.
Mbali na ushindi huo, Tanzania iliteuliwa katika vipengele saba (7) vya Tuzo za WSIS Prizes 2026, na kufanikiwa kutwaa tuzo mbili, sambamba na kupokea vyeti vya utambuzi kwa miradi mingine iliyofanya vizuri katika sekta ya TEHAMA.
Mradi wa Minara 758 ulizinduliwa rasmi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Aprili 10, 2026 jijini Dodoma.
Leo, mradi huo unatambuliwa Kimataifa kama mfano wa mafanikio katika kupunguza pengo la Kidijitali, kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika uchumi wa kidijitali na kuharakisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu kupitia teknolojia ya mawasiliano.