MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, ameipongeza Wizara ya Ujenzi pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kasi na ubora wa utekelezaji wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, ambao umefikia hatua za mwisho za kukamilika.
Shekimweri ametoa pongezi hizo Julai 8, 2026, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kujionea hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wake.
Amesema ameridhishwa na maendeleo makubwa yaliyopatikana tangu alipotembelea mradi huo mara ya mwisho, akibainisha kuwa miundombinu muhimu imekamilika huku kazi zilizobaki zikiendelea kukamilishwa kwa kasi.
Ameeleza kuwa barabara ya kurukia na kutua ndege (runway), njia za ndege (taxiways) pamoja na mnara wa kuongozea ndege (Control Tower) tayari vimekamilika, huku ujenzi wa jengo la abiria ukiwa katika hatua za mwisho za umaliziaji.
“Niwapongeze sana TANROADS kwa kazi kubwa mnayoifanya. Tumefarijika sana na maelezo tuliyopatiwa kuhusu maendeleo ya mradi huu. Tofauti na ziara yetu ya mwisho, leo tumeshuhudia sehemu nyingi muhimu zikiwa zimekamilika, jambo linaloonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati,” amesema Shekimweri.
Aidha, amewataka TANROADS kuendelea kusimamia ubora wa kazi katika hatua za mwisho za utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na kusisitiza umuhimu wa kuboresha mandhari ya uwanja kwa kutengeneza bustani, kupanda miti na kuhakikisha mazingira yanakuwa ya kuvutia na rafiki kwa watumiaji.
Amesema kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato kutakuwa chachu ya kukuza uchumi wa Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla kupitia kuongezeka kwa fursa za biashara, uwekezaji na utalii, sambamba na kuimarisha huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi.
Pia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa ubora, kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyopangwa.