RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema dhamira ya maridhiano ya kitaifa ni kuwaunganisha wananchi, kuimarisha umoja na mshikamano, na kuweka mazingira bora ya maendeleo ya Zanzibar.
Akizungumza baada ya kushiriki Sala ya Ijumaa na ufunguzi wa Msikiti wa Abrar, Fuoni Kibondeni, Mkoa wa Mjini Magharibi, leo tarehe Julai 10, 2026, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza wananchi kusameheana, kuachana na mifarakano na kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo.
Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa misikiti kutumika kama vituo vya ibada, malezi ya maadili na kutoa elimu dhidi ya changamoto za kijamii.
Aidha, ametoa wito wa kuendelea kuwasaidia mayatima, wajane, watu wenye ulemavu na makundi mengine yenye mahitaji maalumu, huku akiipongeza Taasisi ya Al Hilal Islamic Center kwa ujenzi wa Msikiti wa Abrar.
Baadaye, Rais Dkt. Mwinyi alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi Lumumba na kumjulia hali Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Kichama, Muhammed Rajab Soud aliyelazwa hapo.