Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesema iwapo mchakato wa maridhiano kati ya chama hicho na ACT Wazalendo utaenda vizuri na kukamilika, kasi ya maendeleo itaongezeka zaidi.
Chama hicho kimesema, hivisasa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Mwinyi mambo mengi yamefanyika, hivyo iwapo ACT watakubali kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hatua kubwa zaidi itapigwa Visiwani humu.
Hayo yamesemwa jana Julai 7, 2026 na Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, wakati alipozungumza na waandishi wa habari, kuelekea tukio la tamko la pamoja la maridhiano ya kisiasa baina ya chama hicho tawala na ACT Wazalendo linalotarajia kufanyika Julai 9, 2026, kwenye Viwanja vya Ikulu Zanzibar.
Mbeto alisema, Serikali inafanya wajibu wake katika kuleta maendeleo, lakini Serikali nzuri ni ile ambayo ina ridhaa ya wananchi wote na kwa maana hiyo, itasaidia kutuliza siasa zetu pia kuwa na matumaini ya maendeleo zaidi.
“Tukifikia mahala pazuri, kasi itaongezeka, Serikali nzuri ni ile inayopata ridhaa ya wananchi wote; kwanza itatuliza siasa zetu, itawapa matumaini ya maendeleo wananchi wetu, Wazanzibar na Watanzania wanataka maendeleo, hawahitaji malumbano yetu ya kisiasa,” alisisitiza Mbeto.
Alisema, uchaguzi umefanyika na umekwisha, kinachotakiwa ni kufanya kazi ya kuwatumikia Wazanzibar kwa umoja wao bila kuangalia itikadi zao za vyama, dini na maeneo wanapotoka.
“Hili ni jambo zuri tunatakiwa Watanzania wote tuwaunge mkono viongozi wetu, maana kupata hili tamko la pamoja haikuwa rahisi, lakini watu waliweka mbele maslahi ya Wazanzibar kuliko kitu kingine,” alisema Mbeto.
Mwenezi huyo alisema, hana wasiwasi kila kitu kitakwenda vizuri na yote ambayo watakubaliana yakiwemo yale ambayo yanamuhusu Rais moja kwa moja, yatafanyiwa kazi, lakini yanayohusu mchakato wa sheria nayo yatafuata taratibu husika na kusimamiwa na timu ambazo zinahusisha pande zote mbili.
Katika hatua nyingine, Mbeto alisema tamko hilo si la CCM wala ACT Wazalendo, bali ni la pamoja baina ya vyama vyote viwili na anaamini kuwa linachangia kwa kiasi kikubwa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yanavyotaka.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, iwapo katika Uchaguzi Mkuu, chama ambacho kitashika nafasi ya pili na kupata kuanzia asilimia 10 ya kura zote, kitapata nafasi ya kushiriki kuunda Serikali kwa kutoa Mawaziri na Makamu wa Kwanza wa Rais.