Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimewatoa hofu Watanzania na kuwataka kutembea bila wasiwasi kwasababu vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara na vimeimarisha ulinzi.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 7, 2026 na Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis na kusisitiza kuwa, nchi ina amani na hakuna sababu zozote kwa kuandamana.
Mbeto alisema, hakuna sababu yoyote ya kuharibu amani ya nchi kwa ajili ya kumkataa kiongozi fulani, wakati viongozi husika wanakaa madarakani kwa muda maalumu na ukifika wanaondoka na kuwaachia wengine.
“Kama haumtaki Samia, kawekwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, subiri amalize muda wake ataondoka,” alisema Mbeto na kuongeza kuwa, hata yeye kwenye nafasi yake ya Uenezi, wamepita watu wengi, naye ukifika muda wa kuondoka ataondoka na kumuachia mwingine.
Alisema, hata Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Mwinyi, nao muda wao ukifika wataondoka madarakani, hivyo hakuna sababu ya kuvuruga amani ya nchi: “Tulinde amani ya nchi yetu, hatuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania, tusikubali kuchochewa,”
Mwenezi Mbeto alisema, anafahamu wazi kwamba maandamano ni haki, lakini zipo taratibu zinazopaswa kufuatwa, huku akiweka wazi kwamba, kama kuna mtu ana madai yake, zipo njia za kuyawasilisha, ndio maana zimeundwa Wizara na madawati mbalimbali yanayopokea maoni na madai ya Watanzania.