RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha miaka 30 ya utekelezaji wa majukumu yake, hususan katika kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo Julai 1, 2026, alipohudhuria Hafla ya Tuzo ya Rais kwa Mlipakodi Bora na Maadhimisho ya Miaka 30 ya TRA, iliyofanyika Mlimani City, Jijini Dar es Salaam, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza uongozi na watumishi wa TRA kwa weledi wao, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ulipaji wa kodi kwa hiari, kupanua wigo wa kodi na kuimarisha mazingira rafiki kwa walipakodi.
Vilevile, amewapongeza walipakodi waliotunukiwa Tuzo ya Rais kwa Mlipakodi Bora na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na TRA katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amekabidhi tuzo kwa washindi mbalimbali waliotambuliwa kwa mchango wao katika ulipaji wa kodi na ufanisi wa forodha.
Miongoni mwa washindi hao ni Watu Credit Tanzania Limited, Meta Platforms Ireland Limited, Puma Energy Tanzania Limited, Bakhresa Food Products Limited, Marinair Freights Limited, Toyota Tanzania Limited, Mount Meru Petroleum Limited na DP World.