Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kinaridhishwa na juhudi mahsusi zinazochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzungumza na makundi mbalimbali ndani ya jamii ili kupata suluhu, muafaka na maridhiano ya Kitaifa, ikiwa ni pamoja na kukubali kukutana hivi karibuni na Kamati ya Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Ikulu Chamwino, jijini Dodoma.
Aidha, chama hicho kimebainisha kuwa Dkt. Samia licha ya mazungumzo na wanataaluma, wanasiasa, viongozi mbalimbali wa dini na taasisi zisizo za kiserikali, pia amefanya jambo kubwa la kuelekea Tanzania mpya kwa uundaji wa Tume za Haki Jinai na Tume ya Uchunguzi.
Ufafanuzi wa msimamo huo wa CCM uliotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Komredi Khamis Mbeto Khamis, ulifuatia swali aliloulizwa na wanahabari Ofisini kwake CCM Ofisi Kuu Kisiwandui Unguja, Agosti 15, 2026, hatua zilizofikiwa katika mchakato wa kufikia maridhiano ya Kitaifa.
“Kinachoendelea si ukimya bali masuala yote yanashughulikiwa kwa umuhimu wake, yanaendelea kufanyiwa kazi huku yakifuata taratibu sahihi na thabiti kwa matokeo yatakayoponya,” alisema Mbeto.
Mbeto alisema, Rais Dkt. Samia ana baraka za CCM katika kushughulikia mchakato huo na kuhakikisha makundi yote yanapata nafasi ya kutoa maoni na kusikilizwa na hatua zote anazopitia zinairidhisha CCM.
“Mchakato wa kufikia maridhiano wenye lengo la kuponya yaliyotokea ni kama zege; zege likishachanganywa kwa kokoto, mchanga na saruji halilali. Rais yupo kazini usiku na mchana,” alisema Mwenezi Mbeto na kuwataka Watanzania kuilinda na kuitunza tunu ya amani ambayo Mwenyezi Mungu ameijaalia nchi.
Katika mkutano huo uliofanyika Agosti 10, inaelezwa, pamoja na mambo mengine, Rais Samia na TEC walijadili ushirikiano baina ya Serikali na Kanisa na masuala mbalimbali ya kijamii yakiwemo ya kisiasa.
Katibu Mkuu wa TEC, Dkt. Charles Kitima akizungumza na wanahabari mwanzoni mwa wiki hii, alikiri kufanyika kwa mazungumzo hayo ambayo anasema yaliombwa na TEC na Rais Dkt. Samia aliridhia na kuwaalika, kuwasikiliza, Ikulu Chamwino.
Dkt. Kitima alisema, mapokezi yalikuwa mazuri yaliyojaa undugu na walipewa nafasi ya kuwasilisha mtazamo wao kisiasa nchini ulivyo hivi sasa na jinsi ya kutoka katika hali hiyo na kuombana msamaha na kusameheana ili kuiponya nchi na maaskofu wanashukuru kwa Rais Samia kutenga muda wake na kuzungumza nao.