RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza wazazi na jamii kwa ujumla kuendelea kusimamia malezi ya vijana katika misingi ya imani, ucha Mungu na maadili mema ili kuandaa jamii yenye hofu ya Mwenyezi Mungu na maendeleo endelevu.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito huo leo, Julai 4,2026, katika Maulid ya Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W.) yaliyofanyika katika Viwanja vya Sheikh Sharif Hussein Badawy, Lushoto mkoani Tanga.
Amesema malezi bora ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa familia, jamii na viongozi, akisisitiza kuwa msingi imara wa malezi hujenga taifa lenye amani, maadili na ustawi.
Aidha, amewahimiza waumini kuendeleza tabia njema, maadili mema na kuimarisha mshikamano, upendo na amani kwa ajili ya mafanikio ya dunia na akhera.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito wa kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kudumisha amani, umoja na mshikamano nchini ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amechangia Shilingi milioni 200 kwa ajili ya maendeleo ya Kituo cha Irshad Islamic Center na kuridhia kuwa mlezi wa kituo hicho pamoja na kuidhinisha jina la Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi litumike katika jengo jipya la kituo hicho.
Maulid hayo yamehudhuriwa na maelfu ya waumini, masheikh na wanazuoni kutoka ndani na nje ya Tanzania, na yameendelea kuwa alama muhimu ya kuenzi maisha na mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W.).