Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MAKADA wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokana Mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani, wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa aliyoifanywa tangu alipoingia madarakani.
Walitoa pongezi hizo mara baada ya mafunzo na ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, ambapo wamekiri chini ya uongozi wa Dkt. Mwinyi, yamefanyika mambo makubwa.
Mmoja wa makada hao, Mwalimu Ray Kilongozi kutoka Morogoro alisema, wametembelea bandarini, kwenye shule mbalimbali, viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya michuano ya AFCON, ambapo wameshuhudia maendeleo makubwa.
Kilongozi alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi, pia aliwasihi Wazanzibar kutunza miradi yote ambayo Serikali imewapelekea zikiwemo hospitali ambazo zinatoa huduma zakisasa na kutibu magonjwa ambayo miaka ya nyuma yalikuwa yanatibika nje ya nchi.
“Shukrani za kipekee ziende kwa Dkt. Mwinyi, lakini hatutamsahau Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan Mwenyekiti wa Chama chetu cha Mapinduzi, lakini pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, tunawapongeza sana Wazanzibar kwa ukarimu wao na kutupokea,” alisema Mwalimu Kilongozi.
Naye Fortunata Leonard ambaye ni mshiriki kutoka Singida alisema, mevutiwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Nane hususani kwenye huduma za afya likiwemo suala la utatuzi wa changamoto za magonjwa ya moyo.
“Umefanyika uwekezaji mkubwa, tumeshuhudia vifaa vya kisasa kwa ajili ya matibabu, naipongeza Serikali ambayo imeonyesha ni sikivu na inajipambanua kwa kuleta majawabu kwa ajili ya wananchi wake,” alisema Fortunata.
Alisema, pia wametembelea ujenzi wa bandari ambapo wameona vifaa vya kisasa “tumeona maajabu, pia tumeona viwanja vilivyojengwa vina ubora na kiwango cha kisasa kabisa. Nawapa hamasa wanachama wenzetu hasa waliopo Zanzibar na Bara waone uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.”
Katika hatua nyingine, wanachama hao walipongeza mafunzo ambayo wameyapata ambayo yamewajenga kuwa wazalendo na makada wazuri kwa ajili ya kukisema chama chao na viongozi wao ambao wanafanya kazi nzuri inayoonekana.