MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeendeleza juhudi zake za kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa umma kwa kufanya mkutano maalum na wahariri wa vyombo vya habari, uliolenga kuwajengea uwezo na kuwapatia uelewa wa kina kuhusu utekelezaji wa miradi yake inayotekelezwa nchini kote.
Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF Mhandisi Albert Richard, ameeleza kuwa ushirikiano na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya miradi ya Serikali yanafahamika kwa wananchi huku akiongeza kuwa kupitia wahariri na wanahabari kwa ujumla, ujumbe sahihi kuhusu jitihada za kuboresha miundombinu ya mawasiliano unaweza kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Wahariri walioshiriki mkutano huo walipata fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni pamoja na kujadili namna bora ya kuendelea kushirikiana na UCSAF katika kuhabarisha umma kwa weledi na usahihi.
Kwa upande wake, UCSAF imeahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari ili kuhakikisha taarifa kuhusu miradi yake zinawafikia wananchi kwa uwazi na kwa wakati, hatua itakayochochea uelewa na matumizi ya huduma za mawasiliano nchini.