New York, Marekani
TANZANIA imesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 utaongeza kasi ya kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa kuyajumuisha kikamilifu katika mipango ya muda mfupi, wa kati na wa muda mrefu wa maendeleo ya nchi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo wa kwanza (kushoto) Julai 13, 2026 alipohutubia Mdahalo Mkuu wa Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu la Umoja wa Mataifa la Maendeleo Endelevu (High-Level Political Forum – HLPF) unaoendelea New York, Marekani.
Akiwasilisha tamko la Tanzania katika mdahalo huo, Prof. Mkumbo ameeleza kuwa, pamoja na changamoto zinazoikabili dunia, zikihusisaha mabadiliko ya tabianchi, misukosuko ya uchumi na migogoro ya kikanda, Tanzania imeendelea kupata mafanikio katika utekelezaji wa SDGs.
“Tumeongeza upatikanaji na huduma za maji safi na usafi wa mazingira, kuimarika kwa huduma za afya, kupanuka kwa fursa za elimu bora, kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme, kuharakishwa kwa mageuzi ya kidijitali, uwekezaji katika miundombinu ya kimkakati, pamoja na kuimarika kwa uhamasishaji wa rasilimali za ndani na uwezo wa taasisi za umma” amesema.
Prof. Mkumbo ameongeza kuwa Tanzania inaona Agenda 2030 ikiwa sehemu ya safari ya maendeleo ya muda mrefu, ikifungamanishwa na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), kwa pamoja inaweka msingi wa kuendeleza utekelezaji wa SDGs hata baada ya mwaka 2030.
Alifafanua kuwa, vipaumbele vya utekelezaji katika kipindi kijacho ni pamoja na kilimo cha kisasa, maendeleo ya viwanda, uchumi wa buluu, kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, mageuzi ya kidijitali, maendeleo ya rasilimali watu na uhamasishaji wa rasilimali za ndani ili kuchochea ukuaji jumuishi na endelevu.