Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo wameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya nchi hizo mbili.
Utiaji saini wa Hati hiyo inayohusu ushirikiano katika masuala ya teknolojia (ICT), posta na mawasiliano umefanyika Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Kiserikali ya Rais Tshesikedi nchini Tanzania.
Mkataba huo unaohusu teknolojia umetiwa saini na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania Nape Nnauye, pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya nje wa DRC, Christophe Lutundula.
Tanzania na DRC zimekubaliana kushirikiana na kuendeleza sekta ya mawasiliano kwa kuwa ni sekta pekee inayozalisha rasilimali pamoja na ajira kwa vijana kwa kiasi kikubwa.
Katika kukuza jitihada za biashara kati ya nchi hizo mbili, Rais Samia alisema Serikali ya Tanzania inaifanyia marekebisho meli ya MV Sangara ili ianze tena kutoa huduma ya kusafirisha mizigo kati ya Tanzania na DRC.
Aidha, Rais Samia alisema Tanzania na DRC kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) zina mpango wa kujenga ushoroba wa kati (central corridor) wa barabara itakayounganisha Tanzania na DRC.
Takwimu za biashara baina ya nchi hizo mbili zimepungua kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, hivyo nchi hizo zimefufua Tume ya pamoja ya Ushirikiano ili kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo kwa manufaa ya nchi zote mbili.