TANAPA yaendelea kuaminika Kimataifa

0
Kamishna Mkuu wa Uhifadhi Mussa Kuji

KAMISHNA Mkuu wa Uhifadhi Mussa Kuji amesema, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linaendelea kuaminika na kutambulika zaidi Kimataifa, jambo ambalo linaongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi na vivutio vinavyosimamiwa na Shirika hilo.

TANAPA ni Taasisi ya Umma ambayo ilianzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura ya 412 (National Parks Act Cap. 282) na marekebisho Na. 282 ya 2002 yenye dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yote yaliyotengwa kuwa Hifadhi za Taifa, hadi sasa Shirika hilo linasimamia Hifadhi za Taifa 21 zenye eneo la ukubwa wa Kilomita za mraba 96,908.88 ambalo ni sawa na 10.2% ya eneo lote la nchi.

Akizungumza na Wahariri na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na mafanikio ya Shirika hilo kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye Mkutano ambao umeratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kuji alisema Shirika hilo kutokana na utendaji wake, limepata tuzo mbalimbali.

Akitaja tuzo hizo ni “Best Practice Award” ambayo hutolewa kila mwaka na taasisi ya “European Society for Quality Research – ESQR”. Tuzo hii ya utoaji wa huduma bora Kimataifa, hutolewa kwa ajili ya kutambua taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali pamoja na watu binafsi wanaotoa huduma za ubora wa viwango vya hali ya juu Kimataifa.

Aidha, Kamishna Kuji alisema, TANAPA imepata tuzo zinazotolewa na taasisi ya ESQR kwa kipindi cha miaka minne mfululizo ,ambapo kati ya tuzo hizo, tatu zimepatikana katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kiwango cha “Platinum category” mwaka 2021, “Gold category” mwaka 2022 na “Diamond category” mwaka 2023.

Alisema, Hifadhi ya Taifa Serengeti imepata tuzo inayotolewa na Shirika la “World Travel Awards (WTA)” ya kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa miaka mitano mfululizo (2019 hadi 2023). Tuzo tatu kati ya hizo, tano zimepatikana chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita (tuzo za mwaka 2021 hadi 2023).

“Hifadhi ya Taifa Tarangire na Kilimanjaro zilipata tuzo mara mbili mfululizo kwa mwaka 2021 na 2022 ya kuwa vituo vyenye mvuto katika utalii na Tuzo hizo hutolewa na jukwaa la Kimataifa lijulikanalo kwa jina la “Trip Advisor”.” alisema Kuji.

“Pia kampuni ya Explore Worldwide yenye makao yake makuu nchini Uingereza mwaka huu 2024 imeutambua Mlima Kilimanjaro kuwa namba moja ya Alama za Asili za kudumu na zinazokumbukwa zaidi ulimwenguni (World’s topmost unforgettable natural landmarks).”

Kuji alisema, Tuzo hizo zimeliongezea Shirika kuaminiwa na wateja mbalimbali na kutoa uhakika kwao kuhusu aina ya huduma zitolewazo, kutambulika zaidi na kuongeza idadi ya watalii pamoja na kutoa uhakika kwa watalii na wadau wa utalii kuhusu ubora wa hifadhi.

Sambamba na hilo, filamu ya ‘The Royal Tour,’ ambayo inamuhusisha Rais Samia Suluhu Hassan, nayo imeongeza chachu katika ukuaji wa sekta ya utalii, na kuvutia watalii kutembelea vivutio vilivyopo nchini baada ya kuibuka kwa mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO – 19 ambao ulisababisha kupungua kwa idadi ya watalii.

Alisema, idadi ya watalii ilipungua hadi kufikia 485,827 mwaka 2020, ingawa jitihada zilizofanyika zilisababisha idadi ya watalii kupanda Mwaka 2021/2022 na kufikia watalii 997,873, ambapo hali ya kuimarika kwa utalii nchini iliendelea kupanda ambapo mwaka 2022/2023 idadi ya watalii iliongezeka na kufikia 1,670,437.

“Kufuatia anguko hili la Utalii, Serikali ya Awamu ya Sita ilichukua hatua mbalimbali katika kurejesha hali ya utalii kama ilivyokuwa hapo awali ikiwemo kutengenezwa kwa miongozo maalum (Standard Operating procedures – SOPs) ya kupokea na kuhudumia watalii, na pia kuruhusu upatikanaji wa chanjo ya UVIKO-19,” alisema.

Kuji alisema, katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Machi 19, 2024 idadi ya watalii 1,514,726 (wa ndani wakiwa 721,543 na wa nje wakiwa 793,183) wametembelea Hifadhi za Taifa sawa na ongezeko la asilimia 5%.

Aidha, kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 – Machi 19, 2024 idadi ya watalii 1,514,726 (wa ndani wakiwa 721,543 na wa nje wakiwa 793,183) wametembelea Hifadhi za Taifa sawa na ongezeko la asilimia 5% ikiwa ni zaidi ya lengo la kupokea watalii 1,387,987 (wa nje 827,713 na watalii wa ndani 726,676) katika kipindi husika.

Alisema, idadi ya watalii wanaotarajiwa kutembelea Hifadhi za Taifa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni 1,830,081 (watalii wa nje 963,413 na watalii wa ndani 866,667).

“Katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwepo na ongezeko la siku za kukaa wageni kutoka wastani wa siku 1,749,194 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia wastani wa siku 2,669,586 kufikia Februari 2024 ambalo ongezeko hilo limechangia mapato,” alisema.

Kutokana na ongezeko hilo la watalii wanaotembelea vivutio vya utalii nchini kwa kipindi cha miaka mitatu, mapato ya TANAPA yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 174 (2021/2022) hadi kufikia zaidi ya Shilingi Bilioni 337 kwa mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la Shilingi zaidi ya Bilioni 162 ambayo ni asilimia 94.

Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 (Julai 2023 hadi Machi 19, 2024) Shirika limekusanya zaidi Shilingi Bilioni 340 ukilinganisha na matarajio ya kukusanya zaidi Shilingi Bilioni 295 mpaka Machi 2024.

“Kiasi hiki ni ongezeko la zaidi ya Shilingi ya Bilioni 44 ambayo ni sawa na asilimia 15 huku Shirika lina matarajio ya kukusanya kiasi cha zaidi Shilingi Bilioni 382 hadi Juni 2024,” alisema Kamishna Kuji.

Aliongeza kuwa, “Mapato haya ya sasa yanazidi mapato ya zaidi ya Shilingi Bilioni 282 yaliyokusanywa mwaka 2018/2019 kabla ya janga la UVIKO – 19 ambayo yalikuwa ndio kiwango cha juu cha mapato katika Shirika.”

Aidha, TANAPA imekuwa ikishinda tuzo za hapa nchini ikiwemo ya uandaaji bora wa taarifa za hesabu kwa kufuata viwango vya Kimataifa kwa upande wa taasisi za umma zinazotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).

Shirika limekuwa mshindi wa pili wa tuzo ya uandaaji bora wa taarifa za hesabu za mwaka 2022 katika kundi la Taasisi za Kiserikali zinazotumia mfumo wa IPSASs.

Hata hivyo, mbali na tuzo hizo, mwaka 2018 TANAPA iliingia katika mchakato wa kutambuliwa na Shirika la Viwango Duniani (ISO) ili kujijengea kuaminiwa na wateja, jambo ambalo limechangia kuamini na kuchagua huduma na Shirika hilo na hifadhi zake, hivyo kuongeza idadi ya watalii na mapato.

“Katika miaka mitatu, Shirika limeendelea kutekeleza shughuli za utalii na uhifadhi kwa kuzingatia matakwa ya kiwango cha ubora cha ISO 9001:2015 kinachohusu utoaji wa huduma bora kwa wateja,” alisisitiza Kamishna Mkuu wa Uhifadhi Musa Kuji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here