Na Mwandishi Wetu
JUMUIYA ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) wamekionya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa mtindo wao wa kuingiza siasa kwenye mambo ya msingi yenye manufaa kwa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Rais wa Jumuiya hiyo Frank Nkinda alisema, kwa kipindi kirefu, chama hicho kimejijengea tabia ya kutafuta uungwaji mkono hata katika masuala yasiyo na maslahi kwa Taifa na kupinga mapendekezo yenye dhamira ya kuwaweka watanzania pamoja.
Akitolea mfano wa baadhi ya mambo hayo ikiwemo ripoti ya kikosi kazi iliyokabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa imesheheni mapendekezo mbali mbali yenye tija kwa Taifa letu. “sisi wasomi wa Elimu ya juu hatuoni sababu yoyote ya Chadema kuipinga ripoti hiyo.”
Aliendelea kusema: “Sote tulisikia muhtasari wa kile kilichowasilishwa na Mwenyekiti wa Kikosi kazi, Prof. Rwekaza Mukandala kwa Rais, kwakweli dhamira yake ni njema. Sasa tumeshangaa kakikundi kamoja kamekuja juu na kusema mapendekezo haya hayafai na kwamba ni matumizi mabaya ya fedha za umma,”
Nkinda alisema, Chadema ni miongoni mwa vyama vilivyoitwa kutoka maoni yao mbele ya wajumbe wa Kikosi kazi, lakini wakasusa, “sasa wanataka hata yale yaliyotolewa na watanzania wengine kwa uhuru na haki watu wayapinge,”
Aliongeza kuwa, TAHLISO ambayo ni Taasisi inayolea nguvu kazi ya Taifa, kimsingi wana Mamlaka ya kuonya, kukemea na kushauri mambo mbalimbali katika kuchochea maendeleo ya Taifa.
“Tumesikitishwa na kauli ya Katibu mkuu wa Chadema John Mnyika ya kuita ripoti hiyo kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuwa tu wao walikataa kuwasilisha maoni kwenye kikosi kazi cha Rais,” alisema Nkinda.
Alisema, mtu au taasisi yoyote ya kiungwana ilipaswa kupongeza dhamira iliyoonyeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kutafuta maridhiano ya Kitaifa kwa kupata maoni ya wadau juu ya njia gani za kupita kabla ya kufikia hitimisho na siyo kulalamika mbele ya vyombo vya habari suala alilosema halina msingi wowote.
Aliongeza kuwa, Watanzania wameipokea ripoti hiyo kwa mikono miwili na wanawapongeza wadau wote walioshiriki kutoa maoni kwenye kikosi kazi hicho, wakiwemo wanasiasa mmoja mmoja, vyama vya siasa, viongozi wa dini, viongozi wastaafu wa nchi, wananchi wa kawaida, makundi ya wanazuoni na watu mashuhuri wenye nia njema na nchi yetu.
“Tumeisikiliza taarifa ya Chadema na kuipitia kwa kina na kwa hakika tumegundua ubinafsi, choyo na wivu mkubwa kwa Chama hicho kuona, kwanini Tanzania inaweza ikawa katika maridhiano huku wao wakiwa nje ya mchakato huo, kwa kuwa tunafahamu baada ya wadau wa siasa kukutana Dodoma, chama hicho kilisusia vikao hivyo wakituhumu kuwa hawawezi kukaa meza moja na msajili wa vyama vya siasa kutafuta muafaka” alisema
Alisema, licha ya Chadema kutaka watambulike kama walinzi wa Katiba, lakini wamekuwa watu wa kwanza kudharau Katiba kwa kuamini kuwa vyama vingine ni vidogo na havistahili kutoa maoni yenye kujenga nchi tofauti na wao kitu ambacho siyo cha kiungwana.
“Mlinzi wa Katiba ni kila Mtanzania na sio Chama kimoja cha siasa na Kila mtanzania ana haki sawa mbele ya Sheria” alisema Nkinda.
Aidha, TAHLISO wameitaka Serikali ya Awamu ya Sita isonge mbele, kwakuwa Watanzania wamezinduka na sasa hawapo tayari kusindikiza hoja au matakwa ya wachache kwa Maslahi binafsi.
Sambamba na hayo wametoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulinda demokrasia na kuifanya iwe na maana kwa watanzania, kwa kuzingatia Utanzania, utamaduni, Historia, Mazingira na Maadili.
“Maadili yenye kuweka mbele UTAIFA WETU kabla ya ubinafsi, Maslahi ya jamii kwanza kabla ya Maslahi binafsi,” alisema Nkinda kwa niaba ya Jumuiya hiyo.