Na Mwandishi Wetu
SOKO la Bidhaa nchini (TMX) limeahidi kutoa huduma Kisasa na kujiendesha kwa ufanisi, ili kuhakikisha pande zote zinazotumia jukwaa hilo zinanufaika na maslahi yao yanalindwa.
Aidha, TMX wameahidi kutoa elimu zaidi na kuwafikia wananchi na wakulima ili waweze kunufaika zaidi na Jukwaa hilo ambalo lilizinduliwa rasmi Novemba 30, mwaka 2015 na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Akizungumza na Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya habari nchini Septemba 7, Jijini Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa Tanzania, Godfrey Malekano alisema, wataendelea kufanya utafiti kwa kushirikiana na wadau husika ili kuongeza bidhaa zaidi kwenye soko hilo.
“Dira na dhima ya Soko la Bidhaa ni kuwa soko linaloongoza kwa kutoa huduma za Kisasa, zenye ufanisi kwa uwazi na uadilifu kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu katika kutekeleza na kutimiza malengo ya maendeleo ya Taifa.” alisema Malekano.
Akifafanua kuhusu Soko la Bidhaa, Malekano alisema ni mfumo rasmi unaowakutanisha wauzaji na wanunuzi kwa pamoja na kufanya biashara kupitia Mfumo wa Kidijitali na kuweka wazi kwamba, hadi sasa hakuna malalamiko yoyote ya watu kutapeliwa.
“Soko hili huleta wanunuzi wengi wa ndani na nje ya nchi ambao sio lazima wafike kwenye soko la bidhaa au nchini kwa kuwa mauzo katika Soko la Bidhaa hufanyika kwa kutumia Mfumo wa Kidijitali,”
“Hakuna Mkulima aliyewahi kutapeliwa, wote wanalipwa kulingana na mauzo waliyoyafanya, kwenye hela hakuna tatizo, tatizo lipo kwenye mazao, mtu anasema mazao yake ni ‘Grade A’ ukiangalia unakuta ni kinyume. Kwahiyo kuna haja ya kuangalia zaidi ubora,”
Alisema, kwasasa Soko la Bidhaa Tanzania linamikiwa na Serikali chini ya Msajili wa Hazina na linasimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, ambapo soko kubwa la bidhaa kwasasa lipo India, ambako wanauza zaidi Korosho, Choroko na mazao mengine, ambapo tangu kuanzishwa kwa soko hilo, zaidi ya tani 135,000 za bidhaa zimeuzwa.
“Soko la Bidhaa ni mfumo rasmi unaowakutanisha wauzaji na wanunuzi kwa pamoja wanafanya biashara, kunakuwa na mikataba ya bidhaa inayotoa uhakika wa ubora, ujazo na malipo,” alisema na kuongeza kuwa, soko la bidhaa sio mnunuzi wa mazao, bali kazi yao ni kuwakutanisha wafanyabiashara na wauzaji wa mazao.
“TMX ni ‘Platform’, tunasimamia soko, hatuhusiki na mauzo, sisi tupo kuangalia kama taratibu zimefuatwa na kuhakikisha taarifa zimefika kwa watu wote.