SMZ kuendelea kuwaenzi viongozi mbalimbali

0
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala bora Haroun Ali Suleiman(WANNE KULIA)akijumuika na Viongozi wa Chama na Serikali pamoja na Wanafamilia katika hafla ya kumuombea Dua aliekuwa Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar Brig. Jenerali Ramadhan Haji Faki ikiwa ni muendelezo wa Maadhimisho ya Wiki ya kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa Waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar hafla iliyofanyika Kijijini kwao Mkwajuni Magombewa Wilaya ya Kaskazini A Unguja.

Na Khairat Moh’d, MAELEZO

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itashirikiana na familia ya waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaombea dua viongozi waliotangulia mbele ya haki.

Hayo ameyasema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma wakati wa ziara ya kusoma dua katika kaburi la Marehemu Pili Khamis Mpera huko Kisiwandui Mjini Unguja.

Alisema, ipo haja ya kuwaombea dua waasisi mbambali kwa michango yao mikubwa kwa kushirikiana na familia zao kwa lengo kukumbukwa na vizazi vijavyo.

Aidha, Hamza ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwaenzi na kuyaendeleza mema yote yalioyafanywa na waasisi hao na kuahidi kuyafanyia kazi kwa maendeleo ya nchi.

Nae ndugu wa familia Hassan Khamis Mpera ametoa shukrani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuandaa halfa hiyo na kutambua michango ya viongozi mbalimbali katika serikali .

Dua hiyo imeongozwa na Sheikh Mohd Ramadhan Khamis kutoka Ofisi ya Kadhi Mkuu wa Zanzibar pamoja na ndugu wa familia na viongozi mbalimbali

Wakati huohuo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema, Jenerali Mstaafu Marehemu Ramadhan Haji Faki alikuwa ni kiongozi mahiri, mchapakazi na mwenye juhudi katika utendaji wake wa kazi.

Akizungumza katika ziara ya kusoma dua katika kaburi la aliyekuwa Waziri Kiongozi wa kwanza wa Zanzibar huko Mkwajuni Mgombewa Wilaya ya Kaskazini A Unguja.

Alisema, Waziri Kiongozi huyo alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuchukua hatua za haraka katika kuleta maendeleo ya nchi.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud alisema, kuzuru makaburi ya Waasisi wa Kitaifa kutasaidia kuukumbusha umma namna viongozi hao walivyofanya kazi kubwa za kizalendo kwa ajili ya kuigomboa nchi katika nyanja mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Jenerali huyo Ali Ramadhan Haji ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuandaa utaratibu huo kwa kuwakumbuka waasisi wa Mapinduzi michango yao katika kujenga taifa bora kwa vizazi vijavyo.

Aidha, wamemuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kushirikiana nao pamoja katika kisomo cha dua kwa kipindi kijacho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here