SERIKALI imekamilisha maandalizi ya kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Africa50 General Shareholders’ Meeting – GSM and Infra for Africa Forum), utakaofanyika Agosti 5 hadi 6, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari hukusu Mkutano huo unaotarajiwa kukutanisha zaidi ya washiriki 1,200 kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika, wakiwemo Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa taasisi za fedha za kimataifa, wawekezaji, wanahisa wa Africa50, viongozi wa sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo.
“Maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mkutano huu yamekamilika kwa ushirikiano wa Serikali kupitia wizara mbalimbali, taasisi zake, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau wengine, ili kuhakikisha wageni wote wanapata huduma bora katika mazingira salama na yenye viwango vya kimataifa” alisisitiza.
Chalamila alisema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, atakuwa mwenyeji wa mkutano huo na anatarajiwa kuongoza hafla ya ufunguzi itakayowakutanisha viongozi wa ngazi za juu kutoka Mataifa mbalimbali ya Afrika, akiwemo Rais wa Angola, João Lourenço, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, Rais wa Msumbiji, Daniel Francisco Chapo, Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, Rais wa Kenya, William Samoei Ruto na Rais wa Gabon, Clotaire Oligui Nguema.
Alisema Mkutano huo ni moja ya majukwaa makubwa zaidi ya mwaka 2026 yanayolenga kuharakisha maendeleo ya miundombinu barani Afrika kupitia ushirikiano kati yaSekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), huku ukiipa Tanzania fursa ya kujitangaza kwa wawekezaji wa kimataifa kama kitovu cha biashara, uwekezaji na huduma za usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Mkutano huu unatoa fursa adhimu kwa Tanzania kuonesha uwezo wake wa kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa na wakati huo huo kuwasilisha miradi ya kimkakati inayohitaji uwekezaji mkubwa kutoka sekta binafsi na taasisi za fedha za kimataifa,” alibainisha Chalamila.
Mkuu wa Mkoa huyo alisema Serikali itaitumia fursa hiyo kuwasilisha miradi ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), Bandari ya Dar es Salaam, miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme pamoja na miundombinu ya TEHAMA, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutekeleza Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV) na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesisitiza kuwa mkutano huo hautakuwa na manufaa katika sekta ya uwekezaji pekee, bali pia utachochea ukuaji wa uchumi wa ndani kupitia ongezeko la mahitaji ya huduma za hoteli, usafiri, utalii, migahawa, biashara na huduma nyingine zinazotolewa na sekta binafsi, hatua itakayowanufaisha wafanyabiashara wakubwa na wadogo pamoja na kuongeza mapato ya Serikali.
Aidha, amewaagiza wananchi wa Dar es Salaam kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuwapokea wageni kwa ukarimu, kudumisha usafi wa mazingira na kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa utulivu na mafanikio.
Chalamila pia amewahimiza wafanyabiashara, wamiliki wa hoteli, migahawa, kampuni za usafiri na watoa huduma wengine kutumia fursa hiyo kutoa huduma bora, zenye weledi na uadilifu, huku wakiepuka vitendo vya kupandisha bei visivyo halali ambavyo vinaweza kuathiri taswira ya Tanzania.
Pia, amevitaka vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu mkutano huo ili kuendelea kuitangaza Tanzania kama Taifa lenye amani, mazingira rafiki kwa uwekezaji na uwezo wa kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa.
Mkutano wa Africa50 unatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania mwaka 2026, ukifungua milango ya uwekezaji mpya, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, pamoja na kuongeza nafasi ya Dar es Salaam kama lango la biashara na maendeleo ya miundombinu kwa Bara la Afrika.