RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na Sekta Binafsi ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kujenga Tanzania yenye uchumi shindani, jumuishi na unaojitegemea.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo aliposhiriki Mkutano wa Mazungumzo Maalum kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Sekta Binafsi kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Rais Dkt. Mwinyi amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi na msukumo anaoutoa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inaweka mwelekeo wa maendeleo ya Tanzania na ustawi wa wananchi kuelekea mwaka 2050.
Aidha, amesema Dira hiyo inaweka msingi wa kujenga uchumi unaozingatia tija, ubunifu, matumizi ya teknolojia na ushiriki mkubwa wa Sekta Binafsi.
Amesisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika viwanda, biashara, utalii, uchumi wa buluu, kilimo cha kisasa, huduma za kifedha, uchumi wa kidijitali pamoja na maendeleo ya rasilimali watu.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kushirikiana kikamilifu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha maeneo ya kimkakati yanapewa kipaumbele katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Sambamba na hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua nyenzo za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kushuhudia utiaji saini wa matamko ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika utekelezaji wake.
Miongoni mwa waliosaini matamko hayo ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Juma Malik Akil, kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.