Serikali yafafanua kuhusu nishati safi ya kupikia

0

Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Nishati imewatoa hofu wadau wa sekta binafsi kuwa Serikali inathamini mchango wa matumizi yote ya nishati safi ya kupikia ikiwemo umeme, gesi, na nishati zingine zote ambazo ni rafiki kwa mazingira na afya.

Hayo yamesemwa na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme wa Wizara hiyo, Styden Rwebangila, aliyemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba kwenye mjadala wa wadau hao wa sekta ya nishati ambao wamejadili na kutathmini üelekeo wa sekta ya Nishati.

“Napenda kuwatoa hofu wadau wa sekta binafsi na watanzania kuwa nishati safi ya kupikia  inajumuisha nishati zote na siyo gesi pekee kama wengine wanavyodhani,’’ alisema Kamishna Rwebangila.

Alisema, Wizara ya Nishati inathamini mchango unaotolewa na wadau wa maendeleo hususani Umoja wa Ulaya kwa kufadhili miradi mbalimbali kwenye sekta ya nishati hususani nishati safi ya kupikia na itaendelea kushirikiana nao kwenye upangaji wa mipango mkakati na uendelezaji wa sera.

Nao Umoja wa Ulaya (EU), umeahidi kuendelea kufadhili miradi ya nishati safi ya kupikia kupitia mfuko maalumu wa nishati safi ili kuiwezesha serikali ya Tanzania kufikia malengo yake.

Malengo ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia niashati safi ya kupikia na kuachana na mkaa.

Ahadi hiyo imetolewa leo na Meneja Mradi wa Nishati kutoka Umoja wa Ulaya, Massimiliano Pedretti wakati akizungumza kwenye mkutano huo.

Alisema, watafanya hivyo kuunga mkono juhudi za Serikali katika mkakati  na utekelezaji kufikia azma ya asilimia 80 ya watanzania kutumia nishati safi ifikapo 2034.

Alisema, ili Tanzania iweze kufikia azma yake ni lazima ichukue jitihada za makusudi kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa wauzaji wa mitungi ya gesi, watengenezaji wa majiko ya umeme ili kuchochea wananchi kutumia nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu na upatikanaji wa haraka.

Tayari mradi wa mfuko maalumu wa  nishati  safi ya kupikia unafanya kazi na Wizara ya Nishati ili kuhakikisha taasisi kama Magereza, shule, hospitali kupitia Wakala wa Nishati  REA wanafanya kazi kwa pamoja na kuweka miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwenye maeneo yao.

Naye Meneja mradi wa matumizi bora ya umeme kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa  (UNDP), Aaron Cunningham, alisema UNDP iliamua kuunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania kwenye sekta ya nishati safi ya kupikia kwa kuhakikisha pia inaanzisha programu hiyo ili kuwe na matumizi bora ya nishati ya umeme kwenye Vifaa vitakavyotumiwa na wadau.

Aliongeza kuwa, tayari wameshaainisha viwango vtakavyotumiwa kwenye bidhaa aina tano kama vipoza umeme, Jokofu, Televisheni, Feni,na majiko ya umeme ili vitumie umeme kidogo.

Alisema, mradi huu unatekelezwa kwa pamoja na Wizara ya Nishati tangu walipoanzisha mwaka 2022  na wamekuwa bega kwa  bega na Shirika la Viwango Tanzania TBS ili viwango hivyo vitoe unafuu wa matumizi ya Umeme kwenye vifaa hivyo.

Umoja wa Ulaya umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa kwenye bajeti na miradi ya maendeleo hususani miradi ya Umeme.

Mkutano huo uliohudhuriwa na taasisi zilizoko chini ya Wizara ikiwemo REA, EWURA, TPDC, PURA, TANESCO pamoja na wadau wa maendeleo na sekta binafsi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here