SALIM MOHAMED ZAHORO: Mwanamuziki aliyeacha pengo kwenye Muziki wa rumba nchini

0

Na Mohamed Bakari

MWANAMUZIKI mkongwe wa miondoko ya rumba, Salim Mohamed Zahoro alifariki dunia Februari 2, 2021, nyumbani kwake Buguruni kwa Mnyamani baada ya kuugua na kuzikwa Februari 3, baada ya sala ya alasiri katika makaburi ya Buguruni, ambapo umati mkubwa ulijitokeza kumsindikiza mwanamuziki huyo.

Salim Mohamed Zahoro, atakumbukwa kwa weledi wake wa kutunga nyimbo zenye kukonga nyoyo ambazo wapenzi wa muziki huu wa rumba wamezifurahia. Ni mwanamuziki wa Ki – Tanzania akiwa ni mtunzi, muimbaji na mpiga gitaa. Alizaliwa mjini Tabora, mwaka 1936 na alisoma katika shule ya Msingi ‘White Fathers,’ Tabora kuanzia mwaka 1944 hadi mwaka 1948, ambapo aliacha masomo yake na kuanza masomo ya dini hapo hapo Tabora.

Baadae akawa mwalimu mzuri wa Kaswida akifundisha madrasa mbali mbali ikiwemo madrasa maarufu ya Injumain karibu na msikiti wa ijumaa mjini Tabora. Tangu utoto wake, Salim Zahoro alikuwa mpenzi wa muziki na mwaka 1953 akawa mmoja wa wanamuziki wa Bendi ya Kiko Kids iliyokuwa na maskani yake Tabora.

Mwanzoni, Mzee Zahoro alianzia na kupiga ‘Bongos,’ lakini baadaye alijifunza kupiga chombo cha ‘Mandolin’ na pia akawa mtunzi mzuri na muimbaji na nyota katika bendi ya Kiko Kids ambayo ilishamiri hasa mwishoni mwa miaka ya 50 hadi bendi hiyo ilipovunjika miaka ya 70, na hiyo ni baada ya wanamuziki wake kadhaa wa bendi hiyo kuondoka.

Licha ya jitihada zake za kutaka kufufua bendi hiyo kwa kuwapa mafunzo wanamuziki wapya, lakini kati ya mwaka 1984 na 1985, Mzee Zahoro alilazimika kuacha masuala ya muziki kutokana na matatizo ya kifamilia ikiwemo kifo cha baba yake, nayeye kuhamia Dar es Salaam.

Kwenye miaka ya 1990 baada ya kuundwa kwa bendi ya Shikamoo Jazz, Mzee Salim Zahoro alirudi tena kwenye muziki akiwa muasisi wa kundi hilo akiwa kiongozi, muimbaji na mpiga gitaa la solo akishirikiana na Wazee wenzake akina John Simon, Juma Mrisho Ngulimba, Kassim Mapili, Bakari Majengo, Ali Adinani, Tungwa, Athumani Manicho na Mponda.

Shikamoo ilianzishwa na Taasisi iliyojulikana kwa jina la ‘Help Age International’ ambayo ilikuwa na Makao Makuu yake nchini Uingereza, ikiwa ni Taasisi maalumu kwa kuwasaidia Wazee. Ni yeye Salum Mohamed Zahoro aliyesababisha kuundwa kwa Shikamoo Jazz.

Kiongozi wa Taasisi hiyo, Muingereza aliyejulikana kwa jina la Ronnie Graham alifika hapa Tanzania mwaka 1994 na akaelekezwa kwa Mzee Salim Zahoro, ambapo Ronnie alimtaka Zahoro aanzishe bendi ya Wazee na alimuahidi angemletea vyombo vya muziki kutoka Ulaya.

Ronnie alivutiwa na Mzee Zahoro pale alipowakusanya watu wazima wenzake na kupiga ‘live’ katika sherehe yake iliyofanyika Dar es Salaam. Zahoro na wenzake walipiga katika sherehe hiyo ambayo ilifana na kumpa hamasa Ronnie kuleta vyombo vya muziki ambavyo alimkabidhi mwanamuziki huyo, ambaye aliwatafuta Wazee wenzake na mwaka 1995 walizindua ‘Shikamoo Jazz.’

Wengine alioshirikiana nao ni Juma Mrisho Ngulimba, Kassim Mapili, Bakari Majengo, Tungwa, Kassim Mponda, Ali Adinani na Athumani Manicho. Kwenye moja ya mahojiano yake, alipotakiwa kuzungumzia hali ya muziki ilivyo nchini, tofauti na wakati wa nyuma, Mzee Zahoro alisema, Muziki wa wakati wao ulikuwa mzuri, kwani nyimbo za kipindi hicho zilikuwa na mvuto.

“Sababu ni kwamba, zamani Wasanii waliumiza vichwa vyao kwa kutunga nyimbo zenye mashairi yenye mvuto, kwa mpangilio wa ala na sauti. Mashairi ya nyimbo za zamani yanaweza kudumu hata kwa miaka hamsini ijayo bila kupoteza ladha na hamu ya kusikiliza,” alisema.

Mwanamuziki huyo mkongwe aliwahi kusema kuwa, amesikitishwa na utaratibu wa sasa wa baadhi ya vituo vya Radio kutopiga nyimbo za zamani za muziki wa dansi na badala yake vimetoa nafasi kubwa kwa nyimbo za Wasani wa Kizazi Kipya. Kwa hili, Mzee Zahoro alihisi kwamba kuna kampeni ya kuua muziki wa dansi wa zamani ili kutoa nafasi kwa muziki wa kizazi kipya kutawala.

Kwa wapenzi na Washabiki wa wakati ule wanakumbuka muziki wa Mzee Zahoro wa miaka ya 1960 na ya mwanzo ya 1970 wakati bendi ya Kiko Kids ikitingisha nchi kwa vibao vyao kama ‘Sili Sishibi, Wamtetea Bure, Umeniasi Mpenzi, Tanganyika na Uhuru na Nakataa Kiko na Nimetunda Tunda Bichi. Hizi ni miongoni mwa tungo zilizoiletea sifa kubwa Bendi hiyo ikiwa ni utunzi wa Salim Zahoro, akiwa ameshirikiana na wanamuziki wenzake wa Kiko Kids akiwemo Hassan Luhende kwenye gitaa la ‘Rhythm’ na Hassan Hamisi kwenye Besi.

Desemba 8, 2018 Jijini Dodoma, Salim Mohamed Zahoro alipewa Tuzo ya Heshima ya Uzalendo na Utaifa katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili katika muziki baada ya kupendekezwa na Kamati ya Tamasha la Muziki na Sanaa za Maonesho Tanzania (KAMUSATA), kupitia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo. Kauli mbiu ikiwa: ‘Kiswahili, Utashi wetu, Uhai wetu.

Salim Zahoro alikuwa ni hazina kubwa ya muziki tuliyokuwa nayo hapa nchini, ambapo vijana wangeweza kujifunza mengi yahusuyo muziki kutoka kwake. Tunampa ‘Hai’ Mzee wetu, Salim Zahoro kwa mchango wake mkubwa wa kuendeleza muziki wa dansi hapa Tanzania. VIVA ZAHORO!

*Mwandishi wa Makala hii anapatikana kwa namba 0658 418 839, barua pepe; mohamedmwatiga@yahoo.com.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here