Sababu tano zinazochangia ugonjwa wa akili kujirudia

0

Na Dkt. Raymond Mgeni

KIPAUMBELE na uwekezaji mkubwa wa jamii unapaswa kuongezwa nguvu dhidi ya elimu kuhusu afya ya akili bila kubagua kundi la wagonjwa wa akili.

Mtu akipata tatizo katika afya ya akili yake, haimuathiri peke yake; bali hata wanaomzunguka, jamii hadi Taifa. Mtu anapoathirika akili, anapoteza nafasi ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali.

Huenda kama angekuwa na afya ya akili, angekuwa na faida kubwa kwa jamii na Taifa, na hali yake ya kawaida inarudi kupitia dawa na tiba za Kisaikolojia. Kufanikisha hili hugharimu pesa na muda.

Ugonjwa wa akili ni moja ya magonjwa yenye kuhitaji matibabu ya kipindi kirefu na wakati mwingine, baadhi ya magonjwa ya akili hudumu na mtu maisha yake yote; Mfano Sikizofrenia na Baipola. Magonjwa kama wasiwasi au Sonona yanapopata matibabu, huenda yatakatibika na mtu akarejea kwenye hali yake ya kawaida.

Hivyo, magonjwa ya akili kujirudia rudia hutokea kwa visa vingi vya wagonjwa wa akili ambao kwa namna moja hufika wakati hulazwa pale hali yao inapokuwa mbaya hususani pale anapoanza kupiga watu, kutishia kuua au kujiumiza mwenyewe.

Kwa kuwa ugonjwa wa akili hukaa muda mrefu, kuna namna moja mtu huchoka kufuata au ufuasi wa dawa na hivyo kuona hakuna haja ya kuendelea na matibabu.

Hilo limekuwapo na nguvu ya kusababisha visa vingi vya magonjwa ya akili kushindwa kutengemaa vizuri sababu ya urudiaji rudiaji wa ugonjwa unasababisha uchelewevu wa mtu kurejea katika majukumu ya kawaida, kuleta ugumu wa ndugu kuendelea kumshughulikia mgonjwa hadi kufikia hatua wagonjwa wengine kuachwa sababu ndugu wanachoka.

Mbali na hiyo, sababu zipo nyingi ambazo zinachangia ugonjwa wa akili kujirudia rudia. Zipo dalili za awali ambazo mgonjwa mwenyewe huanza kuziona au ndugu wa karibu. Sababu kama mtu kukosa usingizi, kupandwa na hasira za haraka isivyo kawaida, hali za kujitenga au kukosa kuchangamana na wengine.

Hizi ni dalili za awali zinazoweza kutoa ishara kuwa mtu anapaswa aanze kwenda hospitali kupatiwa matibabu lasivyo ugonjwa utajirudia na kuleta athari kubwa zaidi.

Sababu ya kwanza inayochangia kujirudia kwa ugonjwa ni uachaji wa dawa baada ya mgonjwa kujihisi ameshapona au kutafuta tiba mbadala nyinginezo. Hili huchangiwa zaidi pale dalili ambazo zilijitokeza zikachangia mtu kulazwa kuisha baada ya dawa wengi huacha dawa hizo.

Dalili mfano kusikia sauti ambazo hazipo, kuvua nguo na ufahamu kurejea mtu huona haipo sababu au ushawishi wa ndugu wanaomwangalia kuwa na shinikizo la mgonjwa aache dawa. Kuacha dawa kunachangia sana dalili kujirudia tena kwa mgonjwa hasa pale ambapo kaacha dawa na kupitia mkazo.

Pili, ni kuacha kudhuhuria Kliniki ili kuangalia uwezekano wa kupandisha dozi ya dawa hasa pale ambapo katika dozi ndogo ya tiba dawa bado inamsababisha mgonjwa kuendelea kupata dalili za kiugonjwa wa kuchanganyikiwa.

Mtu anapokosa kuhudhuria kliniki kwa sababu mbalimbali ikiwemo umbali, gharama za kumwona daktari au kuhisi mgonjwa kapona kumekuwa kunachangia sana kwa matatizo ya akili kujirudia rudia. Wengi wanapokuwa wameruhusiwa baada ya kutoka wodini hushindwa kufuata taratibu za kurudi kliniki.

Tatu, kuwa na msongo wa mawazo kwa kipindi kirefu ni chanzo kikubwa kinachosababisha ugonjwa wa akili kujirudia rudia. Mtu anapopata changamoto ngumu iwe katika kazi, mahusiano, hali ya kimaisha huchangia kuibua ugonjwa tena.

Hali ngumu za kimaisha haziepukiki ila zinaweza kudhibitiwa vizuri ili mtu asipate kuugua akili yake.

Nne, matumizi ya vilevi au pombe kumekuwa ni sababu ya wagonjwa wengi ambao awali walipata athari za pombe au vilevi mfano bangi kuleta uchanganyikiwaji wa akili. Pombe au vilevi huathiri mtu katika kuchukua dawa zake kwa wakati au pengine siku anazokunywa pombe kusahau kabisa kunywa dawa za akili.

Pombe inasababisha kuzidi kuharibika kwa mfumo wa mtizamo, fikra na hivyo kuchangia zaidi mtu kupata hali ya kuchangikiwa. Tatu pombe inaweza kupelekea mtu kujiingiza katika vitendo hatarishi vya magonjwa, kufungwa, matumizi holela ya pesa yanasababisha matatizo mengine ya akili mfano sonona.

Tano, matukio yenye kuleta huzuni mfano; matukio kama misiba ambapo mgonjwa wa akili anaweza kufiwa na watu wake wa karibu huenda ni wazazi, watoto, ndugu wengine, rafiki au jamaa.

Mtu anaweza kurudiwa na ugonjwa siku chache baadaye ikiwa atashindwa kukubaliana na tukio la msiba lililojitokeza. Ndugu wa karibu ni muhimu kutoa faraja au hata mgonjwa kwenda kumwona Msaikolojia ili kuepusha hali ya kujirudia kwa ugonjwa.

Kuzuia kurudia rudia kwa ugonjwa ni muhimu kuzingatia haya, ambapo mgonjwa mwenyewe anaweza kushindwa ila wanaomzunguka wakahusika kumsaidia hilo. Ufuasi wa dawa unaweza kusaidiwa na ndugu kukumbusha mgonjwa kunywa dawa zake.

Pia, kukumbusha kurejea tarehe ya kliniki, kumzuia katika kurejea katika unywaji wa pombe, vilevi, kusaidiwa kudhibiti athari za msongo wa mawazo. Mwisho ni ndugu kuishi vizuri na mgonjwa kwa kuepuka unyanyapaa, lugha za kudhalilisha na kunyima haki za mgonjwa wa akili.

0676 559 211

raymondpoet@yahoo.com

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here