Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Oktoba 16, 2022 akiwa Wilayani Kakonko, Mkoani Kigoma amefungua rasmi barabara ya Nyakanazi- Kabingo( km.50) ikiwa imejengwa kwa takriban Shilingi Bilioni 43 na ujenzi wake kusimamiwa na TANROADS.
Akizungumza katika ufunguzi wa barabara hiyo , Rais Samia alisema Serikali imeamua kuifungua barabara hiyo, pamoja na kuweka mawe ya msingi, ikiwa ni juhudi za Serikali za kuleta maendeleo kwa wananchi.
“Tuko katika ziara Mkoani Kigoma, tumeanza na wilaya ya Kakonko, Mradi wa maji Kakonko, Hii ni ishara kubwa Serikali imeamua kuleta maendeleo,” alisema Rais.
Aliongeza ” Ufunguzi wa barabara ya Nyakanazi- Kabingo ni moja ya ahadi za Serikali kurahisisha shughuli za kibiashara kwa wananchi.
Pia, uwepo wa miradi mbalimbali itasaidia kukuza maendeleo kwa wananchi na wananchi waendelee kuchapa kazi kwa bidii”.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Makame Mbarawa alisema ujenzi wa barabara hiyo ni kichocheo kikubwa cha uchumi, na kumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa aliyofanya hadi kukamilika kwa mradi huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa Kakonko wamepongeza juhudi za Rais Samia na Serikali anayoiongoza kwa kuufungua zaidi mkoa wa Kigoma hususan katika sekta ya ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Barabara ya Nyakanazi- Kabingo inaunganisha Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, na Mwanza na pia kuunganisha nchi jirani za Burundi kupitia mpaka wa Manyovu.
Ujenzi wa barabara hiyo ni mkakati wa Serikali kuhakikisha barabara zote zinaunganisha mikoa na nchi jirani, pamoja na zile za ndani zinajengwa kwa kiwango cha lami.