Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
DARAJA jipya la kisasa WAMI ambalo linaunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani pamoja na mikoa ya Kaskazini limeanza kutumika rasmi Oktoba 27, mwaka huu ambapo linakwenda kuwa tija kwa takriban miaka 120 ijayo.
Aidha, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 96 kwa ujumla, asilimia 99 kwa Maendeleo ya kazi za Daraja na asilimia 93 kwa Maendeleo ya kazi za barabara unganishi.
Akikagua daraja hilo lenye M 513.5 na barabara unganishi KM.3.8, lililoanza kutumika na magari kuruhusiwa kupita, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alisema, daraja hilo litafungua uchumi na maendeleo ya wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani na nchi kijumla.
Hata hivyo, alieleza daraja hili linategemewa kupunguza kwa asilimia kubwa ajali za mara kwa mara zilizokuwa zinatokea kwenye daraja la zamani ambalo lilikuwa jembamba na lenye barabara zenye miiinuko mikali.
Alieleza Ujenzi wa daraja jipya una lengo la kutatua changamoto zitokanazo na daraja la zamani ambalo kwa sasa halikidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa kuwa lilijengwa miaka 63 iliyopita (mwaka 1959) .
Mbarawa alifafanua, ujenzi ulianzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano Oktoba, mwaka 2018 chini ya hayati Dkt. John Magufuli na kuacha ujenzi kwa asilimia 44, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekamilisha kwa asilimia 52.
“Sikuja kuzindua nimekuja kupitisha magari katika daraja hili la WAMI, wajibu wetu mkubwa kumshukuru Rais kwa utekelezaji wake na kujivunia Daraja kukamilika,”
“Wapo waliosema miradi inasuasua, haitaendelezwa, lakini leo sisi tunashuhudia utekelezaji wa mradi huu mkubwa, mradi huu ulikuwa ikamilike Novemba mwaka huu, lakini leo Oktoba 27 tunashuhudia daraja limekamilika kabla ya muda, nani Kama Samia?” alifafanua Mbarawa.
Aliwataka wananchi walilinde na kulitunza daraja hilo ili liweze kudumu kwa muda mrefu kama lilivyosanifiwa kufikia miaka 120 ijayo.
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Dorothy Mtenga alisema, maendeleo ya utekelezaji wa mradi umegharimu kiasi cha zaidi ya Bilioni 75, na Mkandarasi alianza kazi rasmi Oktoba 22, mwaka 2018 .
Akizungumzia faida za mradi huo alisema, kiuchumi daraja hilo litaboresha usafirishaji wa bidhaa za viwandani kutoka mikoa ya Pwani na Dar es Salaam ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kaskazini ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na nchi jirani ya Kenya.
Dorothy alisema, kwa upande wa ajira zilizozalishwa, jumla ya ajira 420 kati ya hizo ajira 395 zimetolewa kwa Watanzania na ajira 25 ni za wageni.
Faida nyingine ni kupunguza muda wa kuvuka eneo la daraja kutokana na uwezo wa kupitisha magari mawili kwa wakati mmoja.
“Mradi umesaidia watalaamu wazawa kuongeza ujuzi kutokana na teknolojia mpya ya ujenzi wa madaraja marefu inayoitwa Prestressed Concrete Box Girder – Free Cantilever Method, Teknolojia hiyo kwa hapa nchini bado ni ngeni, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kujenga uwezo na ujuzi utakaolisaidia taifa letu baadae,” alibainisha Dorothy.
Alisema, ujenzi wa daraja jipya la Wami unagharamiwa kwa fedha za Serikali Kuu Shilingi 75, 134, 647,654.55 isiyokuwa na kodi la ongezeko la thamani (VAT). Usanifu uligharimu Shilingi 852, 991,000.00, ujenzi unagharimu Shilingi 67,779,453,717.55, usimamizi unagharimu Shilingi 6,307,484,937.55 na fidia imegharimu Shilingi 194,718,000.00.
Mradi ulifanyiwa upembezi yakinifu na usanifu wa kina na Kampuni ya Intercontinental Consultants and Technocrats Pvt Ltd ya India kwa kushirikiana na Apex Engineering Co.Ltd ya Tanzania kwa gharama ya Shilingi 852,991,000.00 isiyo na VAT mwaka 2016.
Dorothy alisema, kwasasa mkandarasi ataendelea kukarabati daraja la zamani, ambapo baada ya ukarabati litatumika kutokana na maelekezo yatakayotolewa.
Alieleza, daraja jipya lina urefu wa Mita 513.5 kwa kutumia teknolojia ya madaraja marefu, ambapo kuna nguzo kuu nne kati ya hizo mbili zikiwa na urefu wa mita 19.6 na mbili zingine Mita 37.44.1 wakati umbali kutoka katikati ya kila nguzo ni mita 120 na kutoka nguzo za pembezoni na kuta za mwanzo na mwisho wa daraja ni Mita 75.
Daraja lina upana wa Mita 11.85 ambapo kutakuwa na njia mbili za magari za Mita nne kila moja, njia mbili za waenda kwa miguu za Mita 1.5 kwa kila moja na Mita 0.425 za kingo za pembeni ya daraja kwa pande zote.”Daraja litakuwa na taa za mionzi ya jua zenye kamera 21 zikiwekwa umbali wa Mita 25 kila upande.
“Ujenzi wa barabara unganishi yenye urefu wa Kilomita 3.8 ambapo Kilomita 2.1 upande wa Chalinze na Kilomita 1 .7 upande wa Segera kwa kiwango cha lami yenye njia mbili zenye jumla ya upana wa Mita 12 ambapo Mita 3.5 kwa kila njia yapitayo magari, Mita 2 za bega la lami na 0.5 za bega lisilo la lami kila upande,”
Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kufanikisha kukamilisha daraja hilo ambalo limekamilika ndani ya muda.
Alieleza, changamoto kubwa ya muda mrefu tangu mwaka 2014 na kilio cha Watanzania wanaoishi mikoa ya Kaskazini ilikuwa ufinyu wa daraja hilo ambayo sasa imebakia historia.
“Ujio wa daraja hili unakwenda kufungua mwanga mpya katika maendeleo ya wananchi, kwangu mimi napenda kuwaasa wananchi kutunza miundombinu ili liweze kudumu kwa muda mrefu na tuwaonyeshe watanzania kwamba daraja hili kweli tulikuwa tunalihitaji,” alisema Ridhiwani.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainab Abdallah alikemea wale wenye njama ya kudhoofisha jitihada hizo za Serikali, kwa kuharibu miundombinu ya daraja na barabara.
Alieleza, hawatomfumbia macho yeyote atakayebainika kuharibu ama kuiba miundombinu iliyopo.
Akitoa salamu za Chama, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bagamoyo, Abdul Sharif Zahoro aliipongeza Serikali kwa kufanya kazi kwa vitendo.
Sharif alisema, ujenzi wa daraja hilo ni jambo kubwa kiuchumi na kimaendeleo, kwani limefungua fursa mbalimbali na kurahisisha masuala ya usafirishaji.