PPRA yaokoa Trilioni 2.7

0

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema, katika mwaka wa fedha 2023/2024 imeokoa Shilingi Bilioni 14.94 kupitia ukaguzi pamoja na Shilingi Trilioni 2.7 kupitia ufuatiliaji.

Dennis Kwame Simba Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma PPRA alisema hayo wakati wa kikao kazi na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Simba alisema, mpaka kufika Oktoba 31, 2024 jumla ya taasisi nunuzi 21,851 zilisajiliwa na tayari zinatumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).

Alisema, bajeti ya ununuzi ya zaidi ya Shilingi Trilioni 38.6 imewekwa kwenye Mfumo wa NeST, kama fursa ya wazi kwa ajili ya wazabuni.

Vilevile, Mtendaji Mkuu alisema wazabuni wapatao 28,590 wamejisajili kwenye Mfumo wa NeST huku mikataba ya zabuni 62,267 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Trilioni 10.2 imetolewa kwa wazabuni kupitia Mfumo wa NeST.

“Na ununuzi wa umma ni shughuli muhimu ya kiuchumi inayohusisha sehemu kubwa ya Pato la Taifa (GDP) takribani asilimia 70 ya bajeti ya Serikali na taasisi zake hutumika kwenye ununuzi wa umma, hivyo ununuzi wa umma nchini unasimamiwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410.”

Alisema, sheria hiyo imeunda Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa lengo la kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo.

“Chini ya sheria hii zimeundwa Kanuni za Ununuzi wa Umma, 2024 na Miongozo kwa ajili ya kuweka taratibu za ununuzi wa umma. Kanuni mpya za Ununuzi wa Umma zimekwishakamilika,” alisema.

Simba aliongeza kuwa, mamlaka hiyo imewezesha ushiriki wa makundi maalum katika ununuzi wa umma na kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi kwa kuanzisha kanda sita katika mikoa ya Mwanza, Dar es Saalam, Arusha, Mbeya,Tabora na Mtwara.

“Na tumekamilisha ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makao Makuu ya PPRA na kuhamia rasmi tangu mwezi Machi 2024 na hivyo kuokoa pesa ambayo ingetolewa kama kodi ya pango,” alisema Simba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here