Na Iddy Mkwama
MKURUGENZI wa uwezeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Omary Mziya amesema, wanaendelea na mikakati ya kuhakikisha wanaongeza idadi ya wanachama kutoka sekta binafsi.
Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano na Jukwaa la Wahariri (TEF).
Mziya alisema, kundi hilo litahudumiwa kupitia skimu ya Taifa ya hifadhi ya jamii sekta isiyo rasmi (National Informal Sector Scheme – NISS) ambayo ilianzishwa mwaka 2018.
Lengo la mpango huo ni kuongeza wigo kwenye hifadhi ya jamii na makundi yasiyonufaika na huduma hizo pamoja na kuchochea maendeleo na kasi ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Alisema, kwasasa wanaendelea na zoezi la kutoa elimu kwa makundi mbalimbali yajiunge na mpango huo na matarajio yao ni kupata wanachama Milioni 21 kwa siku zijazo.
Mziya alisema, kujiunga na mpango huo ni hiari, hivyo ni lazima kwanza watoe elimu, kisha wahusika wafanye maamuzi na tayari wameshapata wanachama, ingawa bado idadi sio kubwa na wanaendelea kufanya jitihada za kuwafikia wengi zaidi.
“Watanzania wengi wapo kwenye kilimo, ukiangalia kwenye ufugaji nako pia kuna wengi, uvuvi wamejiajiri huko wavuvi wengi sana…lakini kuna wachimbaji wadogo wa madini, hawa wakijiunga itasaidia kupunguza umaskini,” alisema Mziya.
Aidha, Mkurugenzi huyo alitaja makundi mengine ambayo yatanufaika na mpango huo kuwa ni, mafundi, bodaboda, baba na mamantilie na waandishi wa habari, ambapo wanaweza kuchangia Shilingi 1,000 kwa siku ambayo ni sawa na Shilingi 30,000 kwa mwezi.
Alisema, ili kuwapunguzia usumbufu wa kuwasilisha michango kwa makundi hayo, wametengeneza mifumo ambayo wanaweza kulipa wakati wowote na popote alipo.
“Mtu ambaye anafanya biashara yake Kariakoo, kupata muda wa kuwasilisha michango yake ni vigumu, kwahiyo ni lazima umrahisishie na pengine uchangaji wake unaweza kuwa kidogo kidogo,”
“Mfano Shilingi 30,000 ya mwezi hana, ila kila siku ana Shilingi 1,000, 2,000, lazima tukusanye kwa kudunduliza, pia hata kwenye suala la uandikishaji wao tumeweka mfumo mzuri wa kuwarahisishia zoezi hilo,” alisema Mziya.
Mbali na hilo, alisema wameweka mafao kwa ajili ya makundi hayo na yapo ya muda mrefu na muda mfupi; ambapo ya muda mrefu ni uzee, urithi na ulemavu, na mafao ya muda mfupi ni uzazi, matibabu, kujitoa pamoja na msaada wa mazishi.
Mziya, alisema ili kujiunga na mpango huo, ni lazima muhusika awe Mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 15 hadi 70, asiwe mnufaika wa pensheni kwenye mifuko mingine ya hifadhi za jamii na awe na kitambulisho cha NIDA au hati ya kusafiria.
“Ukitimiza vigezo hivyo, unajaza fomu maalumu na kama ni kwenye mfumo wa Kieletroniki, kuna fomu inapatikana huko na kisha ukikamilisha taratibu utaanza kuchanga kidogo kidogo; kwa siku, wiki na mwezi,” alisema Mziya.
Naye Meneja wa mifumo kutoka Mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF) Mihayo Selemani akizungumza kwenye mkutano huo alisema, lengo la matumizi ya TEHAMA kwenye mfuko wa hifadhi hiyo, ni kuhakikisha wanachama wote wanapata huduma zote katika lango la huduma (NSSF Portal).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Deodatus Balile alishukuru NSSF kwa kuandaa mkutano huo, huku akipongeza kuanzishwa kwa mifumo ambayo inawarahisishia wanachama kuwasilisha na kufuatilia michango yao.
Mwenyekiti huyo wa TEF aliipongeza NSSF kwa ujenzi wa daraja la Kigamboni ambalo limesaidia urahisi wa upatikanaji wa huduma za kijamii na kuongeza thamani ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo na kushauri mfuko huo kuwekeza zaidi kwenye miradi mikubwa ya kisasa.