‘NSSF ni mfuko wa uhakika, mimi nauita ni mwajiri wangu’

0
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, akikabidhi tuzo kwa baadhi ya wahariri wastaafu wa vyombo mbalimbali vya habari kwa kutambua mchango mkubwa walioutoa kwa jamii katika kuhabarisha na kuelimisha umma kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo Sekta ya Hifadhi ya Jamii hususan utekelezaji wa majukumu ya NSSF.

Na Mwandishi Wetu

MWANDISHI wa habari mkongwe nchini Frola Wingia amesema, hivi sasa ananufaika na matunda ya kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwani hivi sasa umekuwa kama ndio mwajiri wake kutokana na fedha anazopata kila mwezi.

Akizungumza kwenye Mkutano wa NSSF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa NSSF Mafao House Ilala, Dar es Salaam alisema, ukijiunga na mfumo huo, tayari unakuwa na uhakika wa maisha yako baada ya kustaafu.

“Ni mfuko wa uhakika, mimi nauita ni mwajiri wangu, kama napata zaidi ya Shilingi Milioni moja kila mwezi, maana yake ni hela nzuri, hata nikikukopa nikikuambia nitakulipa, nitakulipa kweli kwasababu ipo,” alisema Frola na kuwataka wanachama wa mfuko huo kuwa wavumilivu.

Alisema, kwasababu ya kukosa uvumilivu, watu wengine wamekuwa wakijitoa kwenye mfuko huo, jambo ambalo limesababisha hivi sasa wayumbe kiuchumi.

“Kwa ambao hawajajiunga wajiunge na wanaotaka kutoka wasitoke, kikubwa ni uvumilivu. Wavumilie, mimi nimevumilia nimeona matunda yake, nilistaafu mwaka 2019 na sasa ni mwaka wa tano nipo kwenye Mfuko wa Pensheni,” alisema.

Aliendelea kusema: “Kila tarehe 23 au 24 fedha zake zinaingia kwenye akaunti yangu, ni mfuko ambao haubabaishi. Ukishajiunga tu, unakuwa umetoka (umefanikiwa). Kuna wengine walitoka mwaka 1996, sasahivi nawaona wamepata mtikisiko kiuchumi, nawafahamu.”

Aidha, aliendelea kusisitiza umuhimu wa waandishi wa habari hususani vijana kujiunga na mfuko huo, kwani una manufaa mengi ikiwemo kuwasaidia kupata mikopo kwa ajili ya ujenzi na shughuli nyingine za maendeleo baada ya kustaafu.

“Ni mfuko ambao haubabaishi wala usiogope. Hakuna longo longo kwenye NSSF, nimeshuhudia wala sisemi uongo,” alisema Flora Wingia ambaye amehudumu kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini, likiwemo gazeti la Nipashe.

Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile akizungumza kwenye mkutano huo, aliwakumbusha waajiri wa sekta binafsi hasa wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi wao NSSF kwa wakati ili wanapostaafu wapate stahiki zao.

“Leo tumepata bahati tumepata ushuhuda kutoka kwa wastaafu waliokuwa wafanyakazi kutoka katika vyombo vya habari ambao ni wanufaika wa mafao ya kustaafu na pensheni ya kila mwezi; Flora Wingia na Bakari Machumu, wametambuliwa na kupewa tuzo, hili ni jambo zuri,” alisema Balile.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here