NCAA wanadi fursa za uwekezaji kwenye jukwaa la SITE

0

Na Jumbe Abdallah


MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ni moja ya taasisi zinazoshiriki onesho la sita la Kimataifa la utalii (Swahili International tourism EXPO) maarufu kama SITE linalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 21 hadi 23, 2022.

Onesho hilo lililofunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango lilifuatiwa na jukwaa la uwekezaji (Investment Forum) ambapo NCAA imetumia jukwaa hilo kunadi fursa za uwekezaji zinazopatikana katika hifadhi ya Ngorongoro.

Akitoa wasilisho kwenye jukwaa hilo Naibu kamishna wa Uhifadhi Needpeace Wambuya amewakaribisha wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika maeneo ya hoteli za safari, kambi za kudumu za malazi, kambi za malazi za muda mfupi, utalii wa picha, safari za kutumia maputo joto, ujenzi wa makumbusho, utalii wa kuteleza kwenye kamba (Zip lines) na utoaji wa huduma ya chakula cha moto porini (Bush lunch Restaurant).

Naibu Kamishna Wambuya amelieleza jukwaa hilo kuwa, Ngorongoro ni eneo maarufu duniani ambalo linatembelewa na wastani wa wageni 700,000 kwa mwaka (kabla ya UVIKO-19) ambapo zaidi ya asilimia 19.1 ya watalii wote wanaotembelea Tanzania wanatembelea hifadhi hiyo hivyo wawekezaji watakaojitokeza watapata tija kubwa katika uwekezaji wao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here