Naibu Waziri ashtukia ‘upigaji’ ujenzi kituo cha Afya

0

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Festo Dugange ameielekeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuunda timu ya uchunguzi kukagua matumizi ya fedha na usimamizi wa ujenzi wa kituo cha Afya Malengamakali kilichopo Mkulula kata ua Malengamakali halmashauri ya Iringa Vijijini.

Dkt. Dugange ametoa maelekezo hayo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo baada ya kutilia shaka usimamizi wa ujenzi wa kituo hicho ikiwemo majibu yasiyoridhisha kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji, Mganga Mkuu na Mhandisi wa halmashauri hiyo.

“Sijaridhiwa na utekekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Malengamakali na itoshe kusema utekelezaji ni mbaya thamani ya fedha hapa sijaiona kwasababu hakuna jengo lililokamilika kwa asilimia 100, hakuna tathimini ya fedha zilizotumika kwa kila jengo haijulikani kila kitu kimekwenda holelaholela haijulikani kiasi gani watendaji hawako ‘serious’ hakuna ‘commitment’ mhe. Rais ameleta Milioni 500 mwaka 2021 /22″

“Leo tunakaribia mwaka 2024 bado wiki moja watendaji hawana majibu kituo cha Afya hakijakamilika na wananchi wanahitaji huduma na umbali hap ani kilomita 34 kutoka vijiji vingine kuja kupata matibabu hapa leo Mkurugenzi anaongelea kituo kitakamilika Oktoba 2024,” alisema Dkt. Dugange.

Aidha, amemwekeza Tawala mkoa huo hufanya uchunguzi huo mapema iwezekanavyo na kuwasilisha taarifa Ofisi ya Rais TAMISEMI na taarifa isiporidhisha timu nyingine ya uchunguzi itatumwa kutoka Ofisi ya Rais.

“Timu hiyo tunataka iwe na wataalamu ikiwemo wakaguzi wa ndani wa mkoa, TAKUKURU mkiwapata na watu wa CAG waje wachunguze thamani ya fedha iliyoletwa, kazi iliyofanyika na tusiporidhishwa na taarifa hiyo tutaleta timu nyingine na tutachunguza kama DMO pamoja na DED kama mnatusaidia au lah na hatutawavumilia watendaji ambao hawatimizi majukumu yao,” alisema.

Hata hivyo, wananchi wa Kijiji cha Mkulula akiwemo Asia Makambi, Lupumuko Chungu na Magreth Sigila wamesema kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia akina mama wajawazito na wazee wanaosumbuliwa na magonjwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here