Mwambe akabidhi magari kwa shule tatu za Sekondari Masasi

0

Na Jumbe Abdallah

MBUNGE wa Jimbo la Masasi Mjini, Geoffrey Mwambe amekabidhi magari matatu kwa shule za sekondari Sululu, Marika na Temeke Masasi ambayo yatatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za utendaji kwa shule hizo.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Mti Mwiba, Mkuti, Masasi Mjini wakati akikabidhi magari hayo, Mwambe alisema atahakikisha anashirikiana na uongozi wa chama Wilaya, na watendaji wengine wa Serikali, kushughulikia changamoto ambazo zimewasilishwa na wapiga kura wake.

Mwambe alitumia mkutano huo kueleza namna Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassani inavyofanya kazi kwa kuhakikisha changamoto za wananchi ikiwamo barabara, maji, umeme na nyinginezo zinafanyiwa kazi.

“Nawaomba mniunge mkono na kuniombea ili kufanikisha kuijenga Masasi Mpya yenye maendeleo. Tuna mipango mingi ya ikiwemo mradi ya ujenzi wa Shopping Malls (Maduka Tisa), ujenzi wa soko la Kisasa,” alisema Mwambe.

Miradi mingine ni ujenzi wa Stendi ya Kisasa yenye thamani ya Bilioni 5, ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale, ujenzi wa barabara ya Mtwara – Mingoyo – Masasi, ujenzi wa barabara ya Mtwara – Newala – Masasi, “Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya na ya mwanzo yote iko mbioni kuanza kwa kuwa taratibu nyingi zimeshafikia pazuri.”

Aidha, Mwambe alisisitiza haja ya kufanya siasa safi zinazowalenga wananchi, na aliwaomba viongozi wote wa chama kuanzia ngazi ya mashina hadi Wilaya kuwatumikia wananchi ili dhamira ya kuitekeleza ilani ya CCM iweze kutimia.

Magari matatu ambayo yametolewa na mbunge wa Jimbo la Masasi Mjini, Geoffrey Mwambe kwa shule za sekondari Sululu, Marika na Temeke, zilizopo Masasi Mjini.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Masasi Claudia Kitta, alimpongeza mbunge huyo kwa kutokuwa mbinafsi, kwani yote anayoyafanya ni ya kipekee, hivyo anapaswa kuungwa mkono ili kufanikisha ujenzi wa Masasi ya maendeleo.

Naye, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Masasi Mariam Reuben Kasembe aliwaomba wananchi wa Masasi Mjini kumuunga mkono Mbunge Geoffrey Mwambe wao kwa kuwa ana dhamira njema.

“Haya aliyoyafanya ndani ya muda mfupi ni historia kwa Masasi Mjini, hivyo tunapaswa kuwa makini na watu wote wanaohubiri chuki na siasa za makundi,” alisema Mariam.

Aidha, alisisitiza kuwa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Masasi kitasimama bega kwa bega na Mbunge huyo ili kuhakikisha ilani inatekelezwa.

Mwenyekiti huyo amewaagiza watumishi wote kuitumikia CCM na kuwatumikia wananchi wa Masasi Mjini na kusimamia miradi ya Serikali kwa uadilifu mkubwa, kwani yeye jukumu lake kubwa litakuwa kuisimamia Serikali na kuahidi kutocheka na wasioitakia mema Masasi.

Pamoja na hayo, aliwataka wazazi kuguswa na elimu ya watoto wao badala ya kukwepa jukumu lao.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, utendaji wa Geoffrey Mwambe, umemwinua Mwalimu Mustapha Swalehe aliyekuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mgombea Ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, na kutangaza rasmi kuhamia CCM, ambapo alikabidhiwa kadi yake kwenye mkutano huo.

“Sioni sababu ya kubaki Chadema wakati kasi ya utendaji naiona kupitia Mheshimiwa Mbunge Mwambe, hivyo nimeona ni bora niungane nae,” alisema Mwalimu Swalehe.

Mkutano huo mkubwa ulihudhuriwa na wananchi wengi wa Jimbo la Masasi Mjini, ambapo wameonesha kuridhishwa na utendaji wa Mbunge wao ambaye ameandika historia ya kipekee kwa aina ya wabunge waliowahi kuhudumu kwenye Jimbo la Masasi Mjini.

Wananchi wamepongeza utaratibu wa Mbunge wao kuwatembelea mara kwa mara kwa ajili ya kuwapa mrejesho wa masuala mbalimbali, pia kupata nafasi ya kuzungumza na mwakilishi wao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here