Na OR-TAMISEMI
MKURUGENZI wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Mfaume Rashid amesema Mpango wa Taifa Jumuishi wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) uliozinduliwa jana utasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa Serikali na wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya, TAMISEMI kwenye uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Dkt.Rashid alisema gharama za matibabu zitapungua kwa Serikali na wananchi kwa kuwa huduma zote zitakuwa zinatolewa sehemu moja.
“Utekelezaji wa mpango huu unahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu na Tunawashukuru Wizara ya Afya kwa kutushirikisha kuanzia hatua ya uandaaji na katika utekelezaji sisi kama TAMISEMI tutashiriki lakini pia nitoe wito kwa wadau wengine kuungana nasi katika utekelezaji wa mkakati huu,”alisema.
Mkurugenzi huyo alisema, lengo la mkakati huo ni kuongeza ufanisi na kuhakikisha kuwa jitihada, ubunifu na rasilimali za mapambano dhidi ya UKIMWI zinaenda kupambana na Homa ya Ini na Magonjwa ya Ngono.